Habari

Wanawake Kilifi lawamani kukataza waume kupanga uzazi

November 10th, 2019 2 min read

Na MAUREEN ONGALA

WANAWAKE katika Kaunti ya Kilifi wameshutumiwa kwa kuwazuia waume zao kukatwa mirija ya kupitisha mbegu za kiume kama njia mojawapo ya kupanga uzazi.

Kulingana na sheria, wanaume ni sharti wapewe idhini na wake zao kabla ya kukatwa mrija wa kupitisha mbege za kiume, maarufu vasectomy.

Kulingana na Muuguzi Mkuu anayesimamia afya ya uzazi katika Kaunti ya Kilifi, Gladys Etemesi, wanawake wamekataza waume zao kukatwa mirija.

Akizungumza katika mahojiano na Taifa Leo, Bi Etemesi alisema wanawake wanahofia kuwa iwapo wanaume watakatwa mirija huenda wakawa mabwege chumbani.

“Wanawake wanadhani waume zao watashindwa kutekeleza majukumu yao kitandani. Kumekuwa na visa ambapo wanaume wanakuja kukatwa mishipa ya kupitisha mbegu za kiume lakini wake zao wanajitokeza na kuwafokea,” akasema.

Bi Etemesi alisema kukatwa mishipa ya mbegu ya kiume ni tofauti na kuasiwa. .

“Si kweli kwamba wanaume wanaokatwa mishipa wanakuwa mabwege chumbani. Ukweli ni kwamba hawataweza kuzalisha lakini wataendelea kuwatosheleza wake zao kitandani,” akasema Etemesi.

Alisema kuwa wanawake pia wanahofia kuwa huenda waume zao wakanenepa kupindukia sawa na mafahali hivyo kushindwa kutimiza majukumu yao ya ndoa.

“Mwanaume aliyekatwa mrija wa mbegu hutimiza vyema majukumu yake ya kitandani na hufikia kileleni sawa na wanaume wengine. Lakini tofauti iliyoko ni kwamba hawezi kutoa mbegu zinazoweza kuzalisha mwanamke,” akasema.

Alisema wanaume wanaokatwa mrija wa mbegu hawawezi kurekebishwa baadaye watasalia hivyo hadi kifo.

Ni wanaume wawili pekee katika Kaunti ya Kilifi ambao wamejitolea kukatwa mirija ya kupitisha mbege za kiume.

Mmoja wa wanaume hao alichukua hatua hiyo kwa sababu mkewe anaugua kansa ya mfuko wa uzazi hivyo hawezi kumeza dawa ya kupanga uzazi.

Mshirikishi wa Afya ya Uzazi na Vijana wa Kaunti ya Kilifi Kenneth Miriti alisema mwanaume wa kwanza alikatwa mrija mnamo 2003 na mwingine 2012.

Mbali na kuzuiliwa na wake zao, Bw Miriti alisema kuwa baadhi ya wanaume pia hawajitokezi kukatwa mirija kwa sababu wanahofia kudunishwa katika jamii.

Kukatwa mrija wa kupitisha mbegu za kiume ni sawa na mbinu nyinginezo za kupanga uzazi kama vile kumeza tembe, kutumia mipira ya kondomu, nakadhalika.

Wanaume hupanga uzazi kwa kutumia kondomu au kukatwa mirija ilhali wanawake wakimeza tembe, kondomu kati ya mbinu nyinginezo.

‘Kukatwa mrija au kutumia kondomu ni mbinu tu za kupanga uzazi. Kukatwa mrija ndio njia salama zaidi kwani mwanaume hawawezi kutungisha mimba,” akasema Bw Miriti.