Habari Mseto

Wanawake mjini Thika wapiga hatua kwa kuuza asali na vifaa vya kitamaduni

June 20th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KIKUNDI cha wanawake 12 mjini Thika, kimejitolea kuendesha mradi wa kuuza asali na vifaa vya kitamaduni.

Mwenyekiti wake Bi Jane Mugure alisema Jumanne mradi huo wa kipekee wameuendesha kwa zaidi ya miaka saba mfululizo bila kusimama.

“Kwanza mradi unaotupatia mapato mazuri sana ni uuzaji wa asali ambayo imekuja kupendwa sana na wakazi wa Thika na vitongoji vyake,” alisema Bi Mugure.

Alitaja pia uuzaji wa vikapu – aina ya Ciondo – ambavyo hutumika sana na wanawake kubeba chakula na vitu muhimu.

Alitaja pembe za ng’ombe, mugwishu, kama baadhi ya vifaa muhimu wanavyouzwa kwa wingi.

“Biashara hiyo imenoga kweli kwa sababu kila siku watu hufurika hapa kwetu kununua vitu hivyo vyote vilivyotajwa hapa. Wengi wao ni wale hufanya matayarisho ya arusi kwani vitu hivyo vyote huhitajika wakati huo wa harusi,” alisema Bi Mugure.

Bi Esther Wangui ambaye ndiye katibu katika kikundi hicho anasema kwa wakati huu wanamiliki mizinga 200 ya nyuki ambapo hupata asali yenye ubora wa kiwango cha hali ya juu.

Bi Esther Wangui (katikati), katibu wa kikundi cha wanawake cha kuuza asali mjini Thika. Jane Mugure (kushoto) ndiye mwenyekiti. Picha/ Lawrence Ongaro

“Sisi mara nyingi hupata asali yetu kutoka sehemu za Pokot ambako sisi husafiri kuchota na kuleta hapa Thika. Imeweza kutupatia faida kubwa kwa sababu hata bei yetu ya kuuza ni nafuu,” alisema Bi Wangui.

Alisema kwa wakati huu kilo moja ya asali wanauza kwa bei ya Sh300 pekee ambapo watu wengi hupenda asali hiyo kwa sababu ya ubora wake.

Alizidi kueleza kuwa wakati wa kiangazi ndipo asali hupatikana kwa wingi kwa sababu wakati huo ndipo nyuki huingia mizingani kwa wingi.

Lakini alisema majira ya baridi mambo huwa mabaya kwao kwa sababu asali hushikana na kuwa ngumu kama mawe.

Alitaja ukosefu wa ufadhili kama kikwazo kinachofanya wasipige hatua kubwa sana.

“Kile tunachotaka sasa ni kuona ya kwamba tunapata mahali pazuri pa kuhifadhi asali kwa wingi ili kutosheleza mahitaji ya wateja wetu wote. Pia tunataka tuwe na mashine yetu ya kuuwekea lebo ya kuonyesha alama ya kazi yetu. Na la mwisho ni kupata soko kwa wingi ili kutupatia motisha ya kuendeleza kazi hiyo,” alisema Bi Wangui.

Kuwapa ‘sapoti’

Mbunge wa Thika Mhandisi Patrick ‘Jungle’ Wainaina, ambaye alizuru maskani yao ya kuuzia bidhaa zao katika soko kuu la U-shop, alisema atazidi kuwaunga mkono wanawake hao kwa sababu wamepiga teke dhana ya kutafuta kazi na badala yake wakajiajiri wenyewe.

“Mimi tayari nimefurahishwa na jinsi wanawake hawa wanaendesha mradi wa kuuza asali ya nyuki na bidhaa za kitamaduni za Agikuyu. Hata nimewashauri waulizie fedha za Uwezo Fund ili waweze kujiinua nazo kwa kununua vifaa muhimu wanavyohitaji,” alisema Bw Wainaina.

Alitoa changamoto kwa vijana wajiweke pamoja na kuanzisha biashara zao wenyewe mradi tu wawe na jambo muhimu linaloweza kuwasaidia katika malengo yao.

Wanawake hao wamefurahia ahadi waliyopewa na mbunge wao kuwa watafadhiliwa na fedha za Uwezo Fund ili wajiinue kibiashara.

“Iwapo tutapokea fedha hizo bila shaka tutapiga hatua zaidi kwa sababu tutanunua vifaa muhimu vinavyohitajika. Kwa hivyo tunashukuru hatua hiyo,” alisemaBi Wangui.