Wanawake sasa walilia usalama katika kampeni

Wanawake sasa walilia usalama katika kampeni

Na VITALIS KIMUTAI

WANAWAKE wanataka kubuniwa kwa sheria itakayowalinda dhidi ya vurugu wakati wa kampeni za uchaguzi.

“Wagombeaji wanawake wamekuwa wakitishiwa, kupigwa na hata kujeruhiwa lakini wahusika hawajawa wakichukuliwa hatua. Kuzua vurugu dhidi ya wawaniaji wanawake kunafaa kuharamishwa na kufanywa kosa la jinai,” akasema Prof Kamar.

Idadi ndogo ya wanawake, kwa mfano, wamekuwa wakijitoa kuwania wadhifa wa ugavana na urais ikilinganishwa na wanaume.

Katika uchaguzi wa 2017, ni wanawake watatu pekee waliochaguliwa; mwendazake Dkt Joyce Laboso (Bomet), Bi Anne Waiguru (Kirinyaga) na Bi Charity Ngilu (Kitui).

Dkt Laboso alifariki 2019 na kiti chake kutwaliwa na aliyekuwa naibu wake Hillary Barchok.

Wanawake wengi wanatarajiwa kujitokeza kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao ikilinganishwa na 2017.

Kulingana na Prof Kamar, sheria iliyoko hailindi wanawake wanaojitokeza kuwania viti mbalimbali.

“Wagombeaji wa kike wanadhalilishwa kwa kurushiwa matusi na hata kuzushiwa vurugu,” akasema.

Katika kongamano lililofanyika hivi karibuni, mjini Kericho, madiwani maalumu kutoka kaunti 47, walilalamika kuwa wito wao wa kuwepo kwa usawa wakati wa kampeni umepuuzwa.

Prof Kamar alishutumu vyama vya kisiasa kwa kukosa mikakati ya kuhakikisha kuwa kuna usawa wa kijinsia katika orodha ya wawaniaji.

“Inasikitisha sana kwamba vyama vya kisiasa vinatenga wanawake, hasa wakati wa kura za mchujo. Wanawake wametengewa tu nafasi chache za uteuzi badala ya kupewa fursa ya kuwania kwani wana uwezo wa kushinda wanaume,” akasema Prof Kamar.

Juhudi za kuhakikishia kuwa kuna usawa wa kijinsia bungeni kulingana na Katiba, zimegonga mwamba baada ya kushindwa kupitisha miswada kadhaa. Miswada hiyo ililenga kuhakikisha kuwa watu wa jinsia moja hawazidi theluthi mbili.

Rais Uhuru Kenyatta amekataa kutekeleza ushauri aliopewa na aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga aliyemtaka kuvunja Bunge kwa kushindwa kupitisha sheria ya usawa wa kijinsia.

Prof Kamar alisema kuwa wanawake wanafaa kuwekewa mazingira bora ya kuwania viti bila hofu ya kushambuliwa na wapinzani wao.

Kamishna wa Tume ya Usawa wa Kijinsia, Priscilla Nyokabi alisema kuwa wanawake wana nafasi nzuri ya kuwabwaga wanaume, wakipewa mazingira salama.

“Tunafaa kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya wanawake wanachaguliwa bungeni ili kuondoa utata ambao umekuwepo kuhusiana na usawa wa jinsia. Katiba ni sharti itekelezwe na haifai kuchukuliwa kama kitabu tu cha kawaida,” akasema Bw Nyokabi.

Aliwataka madiwani kuwashinikiza magavana kuhakikisha kwamba mawaziri wa kaunti wanaoteuliwa wametimiza matakwa ya Katiba kuhusu usawa wa jinsia.

“Hatufai kuendelea kulia kwamba wanawake tunabaguliwa ilhali tuna uwezo wa kushinikiza usawa kupitia mabunge ya kaunti,” akasema.

Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Ann Nderitu aliwahimiza wanawake kuhakikisha kuwa wanapata nyadhifa ndani ya vyama vya kisiasa na kutumia ushawishi wao kupata tiketi ya kuwania viti.

You can share this post!

Vipusa wa Uingereza kuvaana na Northern Ireland mnamo...

Mtihani manaibu 3 wakiendea ugavana