Habari MsetoSiasa

Wanawake wamsifia Moi kuwafungulia uongozi

February 9th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WANAWAKE mashuhuri nchini Kenya waliohudumu wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa pili wa Kenya Daniel Moi wamemsifu kwa mchango wake wa kulinda haki za wanawake nchini.

Walisema Moi aliweka msingi wa viongozi wanawake kwa kuwajengea wasichana shule za upili kote nchini.

Wanawake hao walisema Moi aliwafungulia akina mama milango ya kushiriki katika uongozi na kufanya maamuzi kuhusu nchi yao.

Walisema Moi aliondoa kasumba kwamba wanawake hawakufaa kuchangia katika maamuzi na utawala wa nchi.

Kwenye taarifa waliyotoa baada ya kutembelea familia ya Moi kuifariji, wanawake hao walisema kwamba ni wakati wa utawala wa Moi ambapo Kenya iliandaa kongamano la tatu la wanawake ulimwenguni.

Kongamano hilo lilifungua macho wanawake na wakaanza kushiriki na kutoa maoni yao kuhusu uongozi wa nchi na masuala muhimu kwa taifa.

Wakiongozwa na waziri wa utumishi wa umma Profesa Margeret Kobia, wanawake hao walimsifu Moi kwa kumteua Bi Nyiva Mwendwa kuwa waziri wa kwanza mwanamke nchini Kenya mwaka wa 1995.

“Wanawake wengine waliteuliwa kushikilia nyadhifa tofauti za uongozi wakiwemo manaibu mawaziri na wenyekiti wa bodi za mashirika ya umma,” alisema Profesa Kobia.

Wakati wa utawala wake, Moi alijenga shule nyingi za wasichana ili kuwezesha wengi wao kupata elimu.Wanawake hao walisema hatua hiyo iliinua wanawake wakafahamu haki zao na kujiimarisha kiuchumi.

“Wanawake wa nchi hii hawatamsahau Moi kwa kuwaunga mkono hasa waliotengwa maeneo ya mashambani kwa kukumbatia shirika la Maendeleo Ya Wanawake ambalo lilibadilisha maisha ya wanawake wengi na familia zao,” alisema aliyekuwa mbunge na naibu waziri Mama Phoebe Asiyo.

Walisema wanawake nchini watamkumbuka Moi kama mzalendo aliyeunganisha nchi.“Kama akina mama wa taifa, tunatambua mchango wake wa kuunganisha nchi,” walisema wanawake hao kwenye taarifa yao.

Miongoni mwa waliokuwa kwenye ujumbe huo ni aliyekuwa mwenyekiti wa miaka mingi wa chama cha Maendeleo ya Wanawake Zipporah Kittony, Phoebe Asiyo, Zipporah Kittony, Nyiva Mwendwa, Profesa Leah Marangu, Dkt Jennifer Riria, Profes Wanjiku Kabira na Rahab Muiu.