Habari Mseto

Wanawake wanne waacha watoto wao katika hospitali Thika

May 25th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WATOTO wachanga wanne wameachwa katika hospitali ya Thika Level 5 na akina mama zao baada ya kuzaliwa.

Inadaiwa wanawake hao wanne walikwenda kujifungua katika hospitali hiyo siku chache zilizopita lakini wauguzi baadaye wakapata mshangao baada ya kupata watoto hao kuachwa bila wa kuwalea.

Afisa mkuu katika hospitali hiyo Dkt Jesse Ngugi amesema bado wanaendelea na uchunguzi kubainisha kile kilitokea na sababu gani wanawake hao walichukua hatua hiyo.

“Hatujaelewa ni vipi mama aliyejifungua mtoto anaweza kuwa na ukatili wa aina hiyo wa kumtema mwana wake aliyemzaa,” alisema Dkt Ngugi.

Hata hivyo, alisema “maradhi ya Covid-19 yamekuja na mambo mengi.”

“Wakati kama huu kuna mambo mengi yanayofanyika katika familia nyingi. Tunaelewa watu wengi hawana fedha. Na hata familia nyingi zinapitia migogoro mingi ya hapa na pale,” alisema daktari huyo.

Alisema hospitali hiyo imeamua kuwapeleka watoto hao katika kituo cha watoto cha Macheo Children’ s Home eneo la Gatuanyaga, Thika Mashariki.

“Kituo hicho kinajulikana kwa kuhifadhi watoto wasio na wazazi na tuna imani ya kwamba watoto hao watapewa malezi mema,” akaeleza.

Alisema wauguzi wa hospitali hiyo watachukua jukumu la kuzuru kituo hicho kila mara ili kuona jinsi wanavyopokea malezi yao.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wanawake wawe makini kuwakubali wana wao wanapojifungua.

“Sio jambo la busara kubeba mimba kwa miezi tisa halafu baadaye umtupe na kumtelekeza mtoto wako. Huo ni unyama wa hali ya juu,” akasema Dkt Ngugi.