Habari

Wanawake wanne wanaswa mjini Thika kwa ukeketaji

November 13th, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WASICHANA wanne wadogo waliokolewa na polisi baada ya kupashwa tohara kisiri mjini Thika.

Afisa mkuu wa polisi wa Thika Magharibi, Bi Beatrice Kiraguri, na kikosi chake, walivamia nyumba moja katika mtaa wa Majengo, Thika na kuwapata wasichana wanne waliokuwa wamefichwa chumbani baada ya kupashwa tohara siku tano zilizopita.

Katika msako huo, maafisa wa polisi waliwanasa wanawake wanne wa asili ya Kisomali ambapo baina yao, wawili walikuwa na watoto wao wawili waliokeketwa.

Bi Kiraguri alisema watoto hao wa kike ni wa kati ya umri wa miaka tisa na 12 na wote wamekuwa wamefungiwa ndani ya chumba fulani ili wasitambulike.

“Hii ni mara ya kwanza kushuhudia kitendo cha aina hiyo lakini washukiwa hao wanne watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.

Alisema watoto hao wa kike waliendelea kuhojiwa na maafisa wa polisi halafu baadaye wakapelekwa hospitalini ili kufanyiwa uchunguzi zaidi kabla ya kupewa hifadhi maalum.

Chifu wa Thika Mjini Bw Simon Kamau, ambaye ndiye aliwajulisha maafisa wa polisi kuhusu kitendo hicho alisema watazidi kufanya msako ili kuwanasa watu ambao wanaendesha ukeketaji kisiri.

“Tayari nilipata ripoti kuwa nyanya wa watoto hao kutoka kijiji cha Kiandutu, Thika ndiye alihusika katika ukeketaji wa watoto hao. Nitaendelea kufanya msako ili kuhakikisha kitendo cha aina hiyo hakiendelei tena eneo hili,” alisema Bw Kamau.

Alisema sheria ni lazima ifuatwe vilivyo na serikali haitakubali tabia ya ukeketaji kuendeshwa mjini Thika.

Wakazi wa mtaa wa Majengo, Thika, waliridhika na hatua hiyo baada ya wanawake hao kunaswa na maafisa wa polisi.

Alisema wakazi wa Majengo ndio walikuwa mstari wa mbele kutambua jambo hilo na baadaye kupiga ripoti kwake.

Wakati huo pia kongamano la kimataifa kuhusu idadi ya watu na maendeleo (ICPD), linaloendelea jijini Nairobi linakashifu maswala ya ukeketaji, na kuangazia ustawi wa jamii na uchumi.

Hata Rais Uhuru Kenyatta amewasisitizia Wakenya haja ya kudumisha utamaduni wa Kiafrika na kukashifu kuhusu ukeketaji akidai ya kwamba unafaa kukomeshwa kabisa.