Habari Mseto

Wanawake wazuiwa kushiriki kung'oa Mugumo uliopandwa na Mzee Moi

October 11th, 2018 2 min read

Na JOSEPH KANYI

WANAWAKE hawataruhusiwa kuhudhuria hafla ya kitamaduni ya kung’oa mti ambao ulipandwa na Rais mstaafu Daniel Arap Moi katika uwanja wa michezo wa Ruring’u, kaunti ya Nyeri.

Mti huo, aina ya Mugumo, umepangiwa kung’olewa mnamo Novemba mwaka huu kutoa nafasi kwa shughuli ya upanuzi wa miti katika uwanja huo.

Akiongea jana wakati alipokagua uwanja huo, Waziri wa Michezo wa Kaunti ya Nyeri Margaret Macharia alisema hata yeye hataruhusiwa kuhudhuria shughuli hiyo.

“Tunaandaa hafla kubwa kwa ajili ya kuuong’oa mti huo kwa sababu tunamheshimu zaidi rais mstaafu, lakini kulingana na tamaduni ya jamii yetu ya Kikuyu wanawake hawaruhusiwi kuwepo wakati wa shughuli hiyo,” akasema.

Akaongeza, “Lakini wakati huu tumeelekeza juhudi zote katika maandalizi ya Mashindano ya Riadha ya Dkt Wahome Gakuru na baada ya hapo tutaandaa halfa hiyo.”

Baada ya kung’olewa kwa mti huo, sehemu yake itapandwa sehemu nyingine tofauti katika uwanja huo wa michezo, Bi Macharia akafichua.

Shughuli hiyo itaongozwa na wazee wa jamii ya Agikuyu kulingana na mila na tamaduni za jamii hiyo.

Kulingana na mila na tamaduni ya jamii ya hiyo mti wa Mugumo huchukuliwa kuwa takatifu, haswa ukiwa ulipandwa na kiongozi au ikiwa ilitumika kuendeshea maombi.

Hii ni kulingana mwanachama wa baraza la wazee wa jamii katika kaunti ya Nyeri Mzee Mathenge wa Iregi.

Mti huo ulipandwa na Mzee Moi mnamo Oktoba 28, 1978 alipozuru Nyeti kwa mara ya kwanza baada ya kuchukua hatamu za uongozi baada ya kifo cha Hayati Mzee Jomo Kenyatta.

Mzee Moi alikuwa akipanda miti katika maeneo mbalimbali ya nchi wakati huo, na hata alianzisha kampeni ya kupanda miti kote nchini. Kauli mbiu ya kampeni hiyo ilikuwa ukikata mti mmoja, panda miti miwili’.

Shughuli ya upanuzi wa uwanja huo unatarajiwa kurejelewa baada ya serikali ya kitaifa kuahidi kutoa fedha za kufadhili mradi kuu kabla ya Desemba mwaka huu.

Akiongea jana katika uwanja huo, Katibu wa Wizara ya Michezo, Bw Kirimo Kaberia alisema serikali itatoa pesa zilizosalia kwa mradi huo kulingana na ahadi iliyotolewa na Rais Uhuru Kenyatta.