Habari Mseto

Wanawake zaidi ya 10,000 Mukuru wapigwa jeki kwa kupewa barakoa za bure

December 11th, 2020 3 min read

Na SAMMY KIMATU

[email protected]

ZAIDI ya wanawake 10,000 kutoka mitaa ya mabanda ya Mukuru, kaunti ya Nairobi walifaidika na msaada wa barakoa bila malipo hapo Alhamisi.

Msaada huo ulitolewa na Chama cha Wanawake Wamiliki wa Biashara (KAWBO).

Hafla hiyo iliongozwa na mwanachama wa Bodi kutoka KAWBO, Bi Grace Njoki. Shughuli hiyo ilifanyika katika kambi ya chifu wa eneo la Mukuru-Nyayo South B katika kaunti ndogo ya Starehe.

Lengo la hafla hiyo ilikuwa kulenga mwanamke anayeishi katika mitaa ya mabanda ilioko kwenye kaunti ya Nairobi ambako viwango vya umaskini viko juu sana kutokana na ukosefu wa ajira.

Bi Njoki alisema alipeana barakoa 3,000 katika mitaa kadhaa ya mabanda ilioko katika lokesheni ya South B. Vilevile, watu wengine 6,000 walinufaika na barakoa katika mtaa wa Dandora Phase 2,3 na 4 sawia na wanawake wengine 3,000 kutoka mtaa wa mabanda wa Mukuru-Reuben ulioko katika Kaunti ndogo ya Embakasi Kusini.

“Tumepeana barakoa 6,000 huko Dandora, zingine 3,000 katika mitaa ya mabanda ilioko kwenye tarafa ya South B, Kadhalika, tuliwapatia wakazi wa mtaa wa mabanda wa Mukuru-Kwa Reuben barakoa 3,000,’’ Bi Njoki akasema.

Aliongeza kuwa wazo lao lilikuwa kupeana barakoa tano kwa kila mama.

“Mwanamke ni nguzo na muhimu katika jamii ndio sababu tunawalenga wanawake walioko katika biashara kwa kuwapa barakoa tano kila mmoja kutumia pamoja na kuwagawia watoto wao,” akanena.

Aliongeza kuwa chama hicho kinafanya kazi kwa kushirikiana na Wanawake wa Umoja wa Mataifa. Alisema zaidi mwanamke anayefanya kazi katika biashara yake ndogo hutangamana na watu wengi kwa hivyo hitaji la barakoa wakati wa huu tumo katika wimbi la pili la janga la Covid-19.

Bi Njoki alibaini kuwa wana nia pia ya kuwafikia watu wenye ulemavu wakati wa shughuli hiyo.

“Tumeona hatua, mikakati na juhudi zilizofanywa na watu tofauti baada ya kuzuka kwa corona lakini bila mafanikio kamilifu ndiposa sisi tumejitolea kuwafikia kuwafikia maskini katika jamii,” alisema.

Aliongeza ya kwamba barakoa hizo zinaweza kutumika tena na zinaweza kuoshwa pia. Kwa hivyo, zinafaa kwa wakaazi wanaoishi mitaani ya mabanda.

Katika hafla hiyo, mwanamke, 56 alisema alifurahi sana kupokea barakoa za bure na kuongeza kuwa hawezi kumudu kununua hata barakoa moja akiwa na chakula cha kutia tumboni.

“Ninauliza, nitanunua barakoa ama nitanunua chapati kwa sababu sina pesa. Ninaishi kwa neema ya Mwenyezi Mungu,” aliwaambia waandishi wa habari kwa sharti la kutotajwa jina.

Mbali na barakoa, chama pia kinafundisha wanawake kutoka mitaa ya Mukuru katika usimamizi wa Biashara na mpango wa ushauri wa kifedha. Kufikia sasa, Bi Njoki alisema wanawake 18 wa Mukuru wamenufaika na mpango huo na sasa wanamiliki na kusimamia biashara zao.

“Tunajikita katika kozi za kupika chakula na kahawa zote mbili za wanawake katika mitaa ya mabanda ya Mukuru,’’ Bi Njoki asema.

Wakati wa hafla hiyo, kulikuwa pia na zoezi la kunyunyiza dawa dhidi ya kuua viini katika ofisi za kaunti.Shughuli ya unyunyizaji dawa iliongozwa na mwakilishi wa idara ya Afya katika kaunti ndigo ya Starehe, Bi Theresa Muchomba. Alibaini kuwa idara hiyo hubyunyiza dawa katika masoko na maeneo mengine ya umma kila Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi. Msaidizi wa Kamishena wa kaunti eneo la South B, Bw Michael Aswani Were aliwaambia wakazi kukumbatia maagizo ya wizara ya afya kuzuia msambao wa virusi vya corona wakati tunakaribia msimu wa sherehe. “Ni wazi corona ipo na inaishi nasi kwa hivyo lazima tuzingatie kanuni za wizara ya afya zaidi mwezi huu wa Desemba amabao ni wa sikukuu na kabla ya shule kufunguliwa mnamo Januari. Tunashirikiana na kukusanyika wakati wa hekaheka za Krismasi na Mwaka Mpya kwa hivyo ni juu yetu kuibuka washindi au tuangamie kwa mauti tukiyapuuza maagizo hayo, ’’ Bw Were alionya. Kando na hayo alisema virusi hivyo vinachukua maisha ya watu wengi na kuleta hofu zaidi katika wimbi la pili ikilinganishwa na hapo awali.

“Tutafanikiwa kushinda vita hivi ikiwa tutazingatia na kudumisha maagizo ya wizara ya afya kwani kinga ni bora kuliko tiba, ’’ Bw Were alisema katika hotuba yake.