Wanawe Mugabe kortini kupinga mwili ufukuliwe

Wanawe Mugabe kortini kupinga mwili ufukuliwe

Na KITSEPILE NYATHI

WATOTO wa aliyekuwa rais wa Zimbabwe, marehemu Robert Mugabe wameenda kortini kupinga agizo la mahakama ya kitamaduni la mwili wa baba yao ufukuliwe.

Chifu Zvimba, mwezi uliopita alimpeleka mjane wa Mugabe, Grace, katika mahakama ya kitamaduni akidai kuwa alikiuka mila na desturi kwa kuzika mumewe nyumbani kwao katika kijiji cha Kutama.

Mahakama ya kitamaduni iliagiza mwili wa Mugabe ufukuliwe na badala yake uzikwe katika makaburi ya mashujaa wa vita vya ukombozi wa taifa hilo miaka ya 1970.

Grace pia alitozwa faini ya ng’ombe watano na mbuzi wawili.

Bi Grace alishtakiwa bila kuwepo mahakamani kwani ni mgonjwa na amekuwa akitibiwa nchini Singapore.

Mahakama ya kitamaduni ilitishia kuchukua hatua zaidi iwapo mabaki ya Mugabe hayatahamishiwa katika makaburi ya mashujaa wa ukombozi kufikia Julai 1, mwaka huu.

Watoto watatu wa Mugabe, Bona, Bellarmine Chatunga na Tinotenda Robert, wamekata rufaa wakisema kuwa mahakama ya kitamaduni haina mamlaka ya kufasri sheria.

Familia ya Mugabe inasema kuwa mahakama ya kitamaduni ilikosea kwa kuamua kesi bila washtakiwa kusikilizwa.

Watatu hao walisema kuwa madai yaliyotolewa na mahakama ya kitamaduni kwamba Mugabe alizikwa ndani ya nyumba hayakuwa ya kweli.

Mugabe alizikwa Septemba 28, 2019 kijijini kwake Kutama wiki chache baada ya kuaga dunia akitibiwa nchini Singapore.

Mugabe alikuwa Rais wa kwanza wa Zimbabwe baada ya nchi hiyo kupata uhuru 1980 hadi 2017 alipong’olewa kwa nguvu kutoka wadhifa huo na wanajeshi na nafasi yake ikachukuliwa na Rais Emmerson Mnangagwa.

Mwaka 1987, alibadilisha katiba ili imruhusu kuwa rais kwa muda zaidi, na kuongeza mamlaka yake.

“Mahakama ya kitamaduni haina mamlaka ya kuagiza kufukuliwa kwa maiti ambayo tayari imezikwa. Vilevile Chifu Zvimba aliingilia eneo ambalo haliko chini yake,” wanasema watoto wa Mugabe katika stakabadhi zao walizowasilisha katika mahakama ya hakimu.

Baadhi ya jamaa wa Mugabe, akiwemo waziri wa zamani Patrick Zhuwao, wameshutumu Rais Mnangagwa kwa kufadhili watu wanaotaka mwili wa Mugabe ufukuliwe ili ufanyiwe matambiko.

Lakini serikali imepuuzilia mbali madai hayo. Serikali na familia ya Mugabe walivutana kwa takribani wiki tatu kuhusu mahali ambapo kiongozi huyo angezikwa.

Familia ilishikilia kuwa Mugabe alikuwa amesema kwamba hakutaka azikwe katika makaburi ya wapiganaji wa ukombozi kwa sababu hangependa kukaribiana na makaburi ya watu walioongoza mapinduzi dhidi ya serikali yake.

You can share this post!

Uhuru kuidhinisha Nakuru kuwa jiji la nne Kenya

Safari Rally itakuwa ‘mnyama’ tofauti na yule tumezoea...