Makala

WANDA AWINO: Niliipenda Sarafina, sasa nalenga kumfikia Angelina Jolie

September 30th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

AKIWA mdogo alitamani kuwa mwigizaji hasa alipotazama filamu iitwayo ‘Sarafina’ ya mwanamaigizo Leleti Khumalo mzawa wa Afrika Kusini.

Wanda Adhiambo Owino anasema msanii huyo ambaye katika uhusika wake alifahamika kama Sarafina alimvutia zaidi jambo lililomtia mori kuwa mwigizaji.

Ingawa amehitimu kwa shahada ya digrii kama mwanahabari katika Chuo Kikuu cha JKUAT ameibuka kati ya wasanii wa kike wanaovumisha tasnia ya uigizaji hapa nchini.

Aidha ni meneja wa mcheshi, MC Hamso na mwigizaji Tony Otieno pia mfanyi biashara. ”ingawa ndiyo nimeanza kucheza ngoma ninapania kukwea milima na mabonde kusudi nifikie levo ya kimataifa angalau nitinge hadhi ya staa wa uigizaji mzawa wa Marekani, Angelina Jolie,” anasema.

Kando na hayo kisura huyu anasukuma gurudumu la brandi yake ‘Wonders Creation Theatre’ aliyoanzisha mwaka huu. Anasema inajihusisha na filamu za kuhamasisha watoto kuhusu madhara ya dawa za kulevya, Virusi vya Ukimwi vile vile maswala ya tabia na dini. Chini ya brandi hiyo amefanikiwa kuzalisha filamu moja kwa jina ‘Matandiko na Consolata.’

Demu huyu aliyezaliwa mwaka 1995 anajivunia kufanya kazi ya maigizo na makundi kadhaa ikiwamo JKUAT Art Flame na Milestone Sterling Theatre kati ya mengine.

Anajivunia kushiriki filamu kama ‘A Doll’s House’ na ‘Kigogo’ zilizopata mpenyo na kupeperushwa kupitia KTN Home Televisheni mwaka huu. Filamu hizo zilizalishwa na kundi la Milestone Sterling Theatre alilojiunga nalo mwaka 2017.

Wakenya wengi hupenda kutazama filamu za kigeni kuliko kazi za wazalendo hali anayodai imechangiwa pakubwa na baadhi yao kutotilia maanani utamadumi wa taifa hili.

”Ni muhimu wazalishaji wa filamu hapa nchini tuwe wabunifu pia tuegemee zaidi utamaduni wetu,” alisema na kuongeza kuwa anahisi hatua hiyo itavutia zaidi wapenzi wa burudani ya maigizo humu nchini pia kutoka mataifa ya kigeni.

Katika mpango mzima anahimiza Wakenya wajitokeze kushabikia sanaa ya waigizaji wazalendo ili kupaisha burudani ya maigizo nchini na kutoa ajira kwa waigizaji wanaokuja.

Anadokeza kuwa Wakenya wanaweza kutazama filamu za wazalendo hasa zinazoangazia maswala ya kifamilia ambazo huonyeshwa kwenye kumbi za kijamii kama Kenya National Theatre na Nairobi Cinema kati zinginezo.

Hapa Afrika anasema anatamani sana kufanya kazi na waigizaji kama Taraji P. Henson mzawa wa Marekani ambaye ameshiriki filamu kama ‘Empire’ na ‘Tyler Perry’s Acrimony,’ kati ya zinginezo.

Pia Angelina Jolie ambaye ameigizaji filamu kibao ikiwamo ‘Salt’ na ‘Maleficent.’ Kwa waigizaji wa humu nchini anasema angependa kufanya kazi nao Catherine Kamau ambaye ameshiriki kipindi cha ‘Mother in Law’ na ‘Sue and Jonnie.’

Pia yupo Lenana Kariba ambaye ameshiriki filamu kama ‘How to find a husband’ na ‘Saints’ kati ya zinginezo. Anataka serikali ipunguze ada inayotoswa wategenezaji filamu ili kuvutia wawakezaji wa kigeni kufanyia shughuli zao hapa nchini na kutoa nafasi za ajira kwa wasanii chipukizi.

Anatoa mwito kwa wapenzi wa burudani ya maigizo wajitokeze kwa wingi kutazama filamu mpya ‘Lusting after Demons’ itakayozinduliwa mwezi Novemba, 23 mwaka huu katika ukumbi wa Nairobi Cinema.

Filamu hiyo ambayo binfasi yupo miongoni mwa washiriki inaendelea kufanyiwa kazi na Milestone Sterling Theatre mwandishi akiwa Tony ‘Tot’ Otieno.

Ili kupata tikiti kuhudhuria uzinduzi huo anasema zinapatikana kupitia mitandao ya kijamii, wandapace adhiambo (Facebook), wandapace19 (Twitter) pia barupepe [email protected].

Anahimiza wasanii wanaoibukia kwenye gemu kuwa uigizaji siyo mteremko unahitaji nidhamu, kujitolea na kujituma bila kulegeza kamba pia kumtegemea Mungu zaidi.

Pia anawaambia kamwe wasipuuze masomo maana ndiyo msingi wa kila jambo wanalofanya. ”Binafsi naweza kusema kuwa ni vyema waigizaji kusomea masuala ya uigizaji ili kupata maarifa zaidi hasa jinsi wanavyoweza kuwa wabunifu katika sekta ya maigizo,” alisema. Pia anadokeza kuwa kwa wakati huu hana mahusiano ya kimapenzi mbali anasaka.