Siasa

Wandani wa Gideon wamkemea Ruto

October 11th, 2020 2 min read

FLORAH KOECH na WYCLIFF KIPSANG

VIONGOZI wandani wa mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi wameendelea kushambulia Naibu Rais William Ruto kuhusiana na vuguvugu lake la “Hustler Movement” analotumia kuwapa makundi ya vijana misaada ya kujiimarisha kimaisha.

Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio na Mbunge wa Tiaty, Bw William Kamket, Jumamosi walipuuzilia mipango hiyo ya Dkt Ruto wakisema ni njama ya kutumia maskini kama ngazi ya kuingia Ikulu 2022.

“Sisi kama viongozi wa Pokot tunataka kumwambia kuwa sisi hatutaki wilbaro tupu. Ukileta wilbaro, lete kama umejaza pesa,” akasema Bw Kamket, aliye mwandani wa Senata Moi.

Bw Poghisio alimshambulia Naibu Rais kwa kile alidai ni kumhujumu bosi wake ambaye ni Rais Uhuru Kenyatta.

“Tunahitaji amani kote nchini. Rais mmoja anafaa kuhudumu wakati mmoja. Huu ni wakati mwafaka kwa Naibu Rais kufahamu kuwa hawezi kumzidi Rais. Yeye ni msaidizi tu wa Rais,” akasema Bw Poghisio ambaye ni Kiongozi wa Wengi katika Seneti.

“Je, Rais amekutuma usambaze wilbaro na toroli au ni mpango wako mwenyewe? Ikiwa hajakupa kibarua hicho basi tulia hadi pale atakapokupa kazi,” akaongeza Seneta Poghisio.

Walikuwa wakizugnguza wakati wa mkutano wa kueneza amani kati ya jamii hasimu za Marakwet na Pokot katika eneo la Kollowa, kaunti ndogo ya Tiaty.

Naibu Rais na Seneta Moi wamekuwa wakivutania ubabe wa kisiasa eneo la Rift Valley kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Vita hivyo vya ubabe vimeleta migawanyiko katika jamii ya Wapokot huku kundi moja linaongozwa na Mabw Poghisio na Kamket likiegemea mrengo wa Seneta Moi.

Kundi lingine linaloongozwa na Gavana John Lonyangapuo na kushirikisha wabunge; Samuel Moroto (Kapenguria), Peter Lechakapong (Sigor) na Mbunge Mwakilishi wa Pokot Magharibi Lilian Tomitom, wamesalia kuwa wandani wa Dkt Ruto.

Hata hivyo, Gavana Lonyangapuo alichaguliwa kwa tiketi ya Kanu.

Dkt Ruto amekuwa akiendesha kile baadhi wanahisi ni kampeni kwa lengo la kumrithi Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Hata hivyo, Seneta Moi hajatangaza waziwazi kuwa atawania urais 2022 lakini duru zasema kuwa Kanu inapanga kuunda muungano na vyama vingine kuelekea kwa lengo la kuunga mkono mgombea urais atakayeungwa mkono na muungano huo.

Kiongozi wa ODM Raila Odinga pia ni miongoni mwa viongozi ambao wamekosoa mpango wa Dkt Ruto wa kuwapiga jeki vijana, akiufananisha na kampeni za mapema.

Wandani wa waziri huyo mkuu wa zamani wametisha kudhamini hoja ya kumwondoa mamlakani Dkt Ruto kwa kile wanachodai ni kumkosea heshima Rais Kenyatta.