Habari Mseto

Wandani wa marehemu Moi wataka ‘Fimbo ya Nyayo’ ikarabatiwe

February 2nd, 2024 2 min read

Na FLORAH KOECH

WANDANI wa aliyekuwa Rais wa pili wa taifa la Kenya, marehemu Daniel Arap Moi, sasa wanataka mnara wa Fimbo ya Nyayo uliohusishwa na utawala wake na upo mjini Kabarnet, Kaunti ya Baringo ukarabatiwe.

Mnara huo ambao ulikuwa ukienziwa sana enzi za utawala wa Moi sasa umetelekezwa huku ukiwa umerushiwa rundiko la takataka.

Mnara huo ulikuwa kati ya mingine ambayo ilijengwa nchini kuadhimisha miaka 10 ya utawala wa kiongozi huyo mnamo 1988.

Zamani waliokuwa wakifika mjini Kabarnet walikuwa wakivutiwa sana na mnara huo na wengi walikuwa wakifika karibu nao ili kupigwa picha.

Mji wa Kabarnet unapatikana katika eneobunge la Baringo ambalo Rais Moi aliliwakilisha kwa zaidi ya miongo miwili bungeni.

Mifuko ya plastiki, karatasi, chupa za pombe ni kati ya takataka ambazo zimetupwa kwenye mnara huo na wanaoketi karibu nao ni vijana walevi na wasiokuwa na kazi za kuwajibikia.

Baadhi ya sehemu za fimbo ya nyayo nazo zimeanguka na hata taa zilizokuwa zimeizunguka hazipo tena. Wakazi hawautilii manani tena na kupiga nao picha kama zamani.

Mzee Moi alipofariki mnamo Februari 2020, mnara huo ulikarabatiwa na serikali ya kaunti kwa heshima yake. Hata hivyo, hakuna aliyeutunza huku taa zikiibwa na baadhi ya vifaa vilivyotumika kuutengeneza vikianguka.

Waliokuwa wandani wa Mzee Moi wakiongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa shirika la Posta, Bw Eric Bett, hawajafurahishwa na hali ya mnara huo na wameshangaa kwa nini umetelekezwa.

“Mnara huo ulijengwa kuadhimisha miaka 10 ya uongozi wa Mzee Moi mnamo 1988 na pia ulijengwa kwenye miji mingine kama Nairobi, Nakuru, Meru na Embu. Inasikitisha kuwa minara hii ikiwemo ile iliyoko Kabarnet imetelekezwa na hii ni aibu sana kwa nchi,” akasema Bw Kibet.

“Huu ndio mji wa nyumbani wa Mzee Moi na sielewi kwa nini hata hapa umetelekezwa. Kuna watu ambao wanahusika na wanastahili kutunza mnara huu ambao ni sehemu ya historia ya nchi,” akaongeza.

Bw Bett aliitaka serikali ya kaunti na ile ya kitaifa zimakinike kukarabati minara ya rungu ya nyayo kote nchini. Aliutaka uongozi wa sasa wa Baringo uongoze kwa mfano katika kutekeleza ukarabati huo.

Bw Lee Njiru ambaye alikuwa msaidizi wa kibinafsi wa Bw Moi kwa muda mrefu, alisema kuwa minara hiyo ilijengwa kwa heshima rais huyo alipokuwa akiadhimisha miaka 10 ya uongozi.

Hata baadhi ya watoto waliozaliwa 1978 alipochokua uongozi walialikwa kwenye ikulu wakati wa maadhimisho hayo.

“Mzee Kenyatta alikuwa akibeba mwengo (mgwisho), Moi naye alikuwa akibeba rungu na ndiyo maana ilijumuishwa kwenye minara ya nyayo. Ni makosa kutelekeza minara hiyo kwa sababu Mzee Moi aliongoza nchi hii kwa miaka 24 na hakuna Rais ambaye atawahi kuongoza kwa muda mrefu hivyo,” akasema.

“Hii ni kwa sababu sasa kuna katiba ambayo inamruhusu rais kuongoza kwa miaka 10 pekee. Viongozi wa sasa wanastahili kuheshimu kile Moi alifanya na kutunza minara yake,” akaongeza.