Siasa

Wandani wa Musalia wapinga Raila kuwania urais

October 20th, 2020 1 min read

Na DERICK LUVEGA

KAMBI ya mwanasiasa Musalia Mudavadi sasa inamtaka kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kubanduka katika kinyang’anyiro cha urais 2022.

Kambi hiyo inadai kuwa kulingana na mkataba wa National Super Alliance (Nasa), Bw Odinga aliahidi kutogombea urais baada ya Uchaguzi wa 2017.

Ingawaje Bw Odinga bado hajatangaza nia yake ya kugombea, Mwakilishi wa Kike Kaunti ya Vihiga, Bi Beatrice Adagala na Mbunge wa Sabatia, Bw Alfred Agoi, walisema Bw Odinga anakula njama kisiri za kufanya jaribio la tano la kunyakua urais.

Walisema Bw Odinga alikuwa amekubali kabla ya chaguzi za 2017 kwamba hatawania tena, iwe atashinda hiyo 2017 au la.

Wanasema wakati umewadia kwa Bw Odinga kujiondoa katika jukwaa la kisiasa, baada ya kumaliza nafasi zake za kujaribu kuiongoza nchi.

Hisia za viongozi hao wawili zimejiri siku chache tu baada ya Bw Mudavadi na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka kushiriki mkutano ambao mengi hayakufahamika kuuhusu.