HabariSiasa

Wandani wa Raila wamshauri ajitose debeni 2022

May 6th, 2018 1 min read

ELISHA OTIENO na RUSHDIE OUDIA

WANDANI wa kisiasa wa Kinara wa upinzani Raila Odinga jana wasisitiza kwamba waziri huyo mkuu wa zamani hatastaafu kutoka jukwaa la kisiasa hivi karibuni bali atakuwa debeni katika uchaguzi wa 2022.

Wakiongozwa na Kiongozi wa wachache kwenye bunge la seneti James Orengo, viongozi hao walisema liwe liwalo lazima Bw Odinga awe debeni mwaka huo.

Wakizungumza katika kijiji cha Piny Oyie, eneobunge la Suna Magharibi katika kaunti ya Migori wakati wa hafla ya makaribisho ya nyumbani ya Mwakilishi wa kike wa kaunti Bi Pamela Odhiambo ambayo ilihudhuriwa na Bw Odinga mwenyewe, walisema kwamba kigogo huyo wa siasa za upinzani yuko tayari kuonana kiume na wawaniaji wengine.

Naibu Rais William Ruto anaongoza orodha ya wawaniaji wengine wanaokimezea mate kiti cha urais.

Jumamosi, Bw Orengo alianzisha mjadala huo wa uchaguzi wa 2022 ingawa katika mazishi ya mwanasiasa Kenneth Matiba Rais Kenyatta na Bw Odinga waliwaonya wanasiasa dhidi ya kuanzisha kampeni za mapema na badala yake wahudumie Wakenya.

Aliposimama kuzungumza, Bw Odinga hakugusia suala hilo na badala yake akatetea maridhiano kati yake na Rais akisema siasa wakati mwingine huhitaji ubunifu na tajriba.

“Mimi ni mwanasiasa mwenye ujuzi anayeipenda nchi hii. Hatungeendelea kusambaratisha nchi ndiposa tuliamua kushirikiana,” akasema Bw Odinga.

Aliwataka wanaouliza kwa nini aliamua kushirikiana na hasimu wake wa kisiasa kubadilisha mtazamo na kujiuliza ni matunda yapi yalitokana na maafikiano hayo.

Aidha Bw Odinga aliwaonya waliofuja fedha za wananchi na kuendelea kuzitoa kama michango katika hafla ya Harambee kwamba watajipata pabaya hivi karibuni.

Viongozi wengine walioandamana na Bw Odinga walionyesha utiifu wao kwake na kumtaka asibabaike katika juhudi zake za kutetea wananchi.