HabariSiasa

Wandani wa Raila wamuomba Uhuru azime ziara za Ruto

September 16th, 2019 2 min read

NA RUSHDIE OUDIA

WANDANI wa kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kutoka  Nyanza wamemrai Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati ili kuzima ziara ya Naibu Rais Dkt William Ruto maeneo mbalimbali ya nchi, wakisema anaendeleza kampeni za mapema za uchaguzi mkuu wa 2022.

Wabunge hao zaidi ya 12 walisema ni wazi Dkt Ruto anashiriki kampeni za mapema licha kudai kila mara japo kwamba ziara zake hazihusu siasa bali utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Wakiongozwa na mbunge wa Seme James Nyikal, wanasiasa hao waliokuwa wakizungumza wakati wa ibada katika Kanisa Katoliki la Reru, eneobunge la Seme, Kaunti ya Kisumu pia walipigia debe ripoti inayosubiriwa ya Jopokazi la Maridhiano maarufu kama BBI, wakisema ndiyo njia pekee ya kuhakikisha jamii ya Waluo inashinda kiti cha Urais wakati murwa ukifika.

Wabunge wengine waliohudhuria ibada hiyo ya Jumapili ni Opondo Kaluma (Homa Bay mjini), Dkt Eve Obara (Kabondo Kasipul), Tom Kajwang (Ruaraka), Jared Okello (Nyando), Tom Odege (Nyatike), Elisha Odhiambo (Gem), Martin Owino (Ndhiwa), Jackline Oduol (mteule) Peter Masara (Suna West) na Mbunge Mwakilishi wa Kike Rozaah Buyu.

Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo ndiye alikuwa wa kwanza kumtaka Rais Kenyatta amkomeshe Dkt Ruto.

“Una mamlaka makubwa Mheshimiwa Rais kumzuia Naibu wako dhidi ya kutangatanga. Naomba ufanye hivyo kwa sababu Dkt Ruto amekuwa akizunguka nchi hii kila wikendi,” akasema Bw Odhiambo.

“Kuna madai kwenye historia kwamba wakati Daniel Arap Moi alikuwa Rais na Mwai Kibaki ambaye alikuwa Naibu wake, alitaka kuelekea Kisumu, Rais Moi alimpigia simu na kumtaka akome kusafiri mara kwa mara na badala yake aketi afisini ili afanye kazi. Rais Kenyatta anafaa kuwajibika na kumdhibiti Naibu wake,” akaongeza Bw Odhiambo huku akisisitiza ziara ya Dkt Ruto maeneo ya Pwani na Magharibi huwa ni za kisiasa.

Bw Masara naye alisifu ushirikiano kati ya Rais na Bw Odinga akisema umeleta amani nchini huku akidai kwamba amani hiyo ipo katika hatari ya kupotea iwapo Dkt Ruto ataruhusiwa kupiga siasa za 2022.

“Hatuwezi kuwapa nafasi za uongozi watu ambao hawaaminiki na hawana lolote jipya la kuwapa raia. Kwa muda wa miaka miwili Dkt Ruto amekuwa akiendesha kampeni kali akimshutumu Bw Odinga kwa kugawanya chama tawala cha Jubilee. Raila siyo tatizo la taifa hili bali ndiye mwokozi wa nchi hii,” akasema Bw Masara.

Bw Kaluma na Bw Kajwang nao walisema taifa hili linaelekea kwenye mkondo wa kuridhisha hasa baada ya maandamano yaliyosababisha mauti katika ngome za upinzani wakat wa uchaguzi tata wa 2017.

Wanasiasa hao pia walisema kwamba Dkt Ruto yupo njiani kuwa kinara wa upinzani nchini 2022 asipobadilisha mbinu zake za kisiasa ambazo hulenga sana Bw Odinga.