HabariSiasa

Wandani wa Ruto njia panda

June 4th, 2020 2 min read

CHARLES WASONGA,  IBRAHIM ORUKO NA WANDERI KAMAU

SIKU chache baada ya Naibu Rais William Ruto kuonekana hadharani na Rais Uhuru Kenyatta wakati wa sherehe za Madaraka Dei, na kuibua matumaini kuwa huenda kuna muafaka fulani baina yao, wandani wa naibu huyo wangali katika njia panda.

Mnamo Jumanne, katika mkutano na wabunge wa Jubilee, viongozi wa kisiasa wanaoegemea mrengo wa Dkt Ruto walivuliwa madaraka hata ingawa Kiongozi wa Wengi Bungeni, Bw Aden Duale alionekana kusazwa.

Na ingawaje Bw Duale alisazwa, kuna dukuduku kwamba bado anaandamwa kutokana na uhusiano wake na Dkt Ruto.

Na jana Kiranja mpya wa Wengi Emmanuel Wangwe alitoa ilani ya kufurusha wabunge wanne wandani wa Dk Ruto kutoka kamati za bunge, miongoni mwao akiwa Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na mwenzake wa Kikuyu Kimani Ichung’wa.

Wabunge wa mrengo wa Kieleweke wanaendesha mikakati ya kumwondoa Bw Duale kupitia hoja bungeni au katika mkutano wa kundi la wabunge wa Jubilee ulioratibiwa kufanyika baada ya majuma matatu.

Wanasema kampeni za kuwalemaza wandani wa Dkt Ruto hazitakamilika ikiwa Bw Duale ataendelea kushikilia wadhifa huo.

“Ndiyo mambo bado kwa Duale. Haitakuwa na maana yoyote kwa Kipchumba Murkomen, Susan Kihika, na Kithure Kindiki kupokonywa nyadhifa zao katika Seneti lakini Duale aendelee kuhudumu katika uongozi wa bunge la kitaifa,” akasema Mbunge wa Tiaty, Bw William Kamket.

Naye Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu alisema ingawa alitaka Duale ang’olewe, hakuwa na lingine ila kuheshimu msimamo wa chama cha Jubilee.

“Japo nilishinikiza aondolewe, uamuzi wa chama na kiongozi wake ni kwamba asalie. Ninaunga msimamo wa kiongozi wa chama na ninamtakia Duale kila la heri,” akaandika kwenye Facebook.

Hata hivyo, Bw Duale amepuuzilia mbali madai kwamba angali anakabiliwa na hatari ya kupoteza kiti hicho, akisema “huo ni uvumi ambao hauna msingi wowote”.

Lakini hayo yakijiri, kimya chake Dkt Ruto kiliwachemsha pia baadhi ya wandani wake, wakisema kuwa hawaelewi kwa nini amenyamaza wao wakigongwa.

Aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa alimshtumu Rais kwa kimya chake baada ya mbunge wa Mumias Mashariki, kung’olewa kama Kiranja wa Wengi.

“Nina hakika ikiwa Bw Ruto angemsihi Rais, Bw Washiali angenusurika shoka,” alisema Bw Echesa akipuuzilia mbali madai kuwa mabadiliko hayo yalichangiwa na katibu mkuu wa Cotu, Bw Francis Atwoli am Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya.

Na jana wandani wengine wa Naibu Rais waliopokezwa barua ya kuwaondoa kutoka kamati za bunge ni Mbunge Mwakilishi wa Bomet Joyce Korir, Robert Pukose (Endebess) na mbunge wa Aldai Cornel Serem.

Afisi ya Rais

Bw Ichung’wa ataondolewa kutoka kamati ya bajeti ambako anashikilia wadhifa wa mwenyekiti huku Bw Kuria na Pukose wakiondolewa kutoka kamati za uchukuzi na kawi, mtawalia.

Bi Korir anatarajiwa kupoteza nafasi yake katika kamati ya Leba huku Bw Serem akiondolewa kutoka kamati ya Biashara.

Kwingineko, Rais Uhuru Kenyatta jana alifanya mageuzi kwenye mpangilio wa Serikali ya Kitaifa, ambapo Afisi ya Naibu Rais sasa itakuwa chini ya usimamizi wa Afisi ya Rais.

Kwenye mpangilio wa awali, afisi ya Naibu Rais ilijisimamia kivyake.

Kwenye agizo hilo alilotoa jana, hilo linamaanisha kuwa Afisi ya Naibu Rais haitakuwa na uhuru wa kuwaajiri wafanyakazi wake wala kujisimamia, bali majukumu hayo sasa yataendeshwa na Tume ya Kuwaajiri Wafanyakazi wa