MakalaSiasa

Wandani wa Ruto sasa wamuonya Murathe

September 5th, 2020 2 min read

SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

WANDANI wa Naibu Rais William Ruto wamemwonya Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe dhidi ya kuingiza jina la naibu huyo wa rais katika sakata inayozonga Mamlaka ya Usambazaji Dawa Nchini (Kemsa).

Bw Murathe Ijumaa alihojiwa na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) jijini Nairobi kuhusu uhusiano wake na kampuni ya Kiling Limited iliyopewa zabuni ya kuisambazia Kemsa vifaa 450,000 vya kujikinga dhidi ya Covid-19 (PPEs) na ikalipwa Sh4 bilioni.

Hii ni baada ya madai kuibuka kwamba yeye ni mmoja wa wasimamizi wa akaunti za kampuni hiyo inayomilikiwa na kakake mwanahabari Tony Gachoka, Wilbroad Gachoka na mwanamume mmoja mwa jina Zhu.

Lakini badala yake Bw Murathe alidai Dkt Ruto alinunua hisa katika Kilig Limited na akawataka maafisa wa EACC na Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kumhoji naibu huyo wa rais kuhusiana na sakata hiyo.

Vile vile, aliwataka wapelelezi kuwaamuru maseneta wa zamani Boni Khalwale (Kakamega) na Johnstone Muthama (Machakos) kufika mbele ya waelezee wanachofahamu kuhusiana na sakata hiyo.

Akiongea na wanahabari baada ya kuhojiwa kwa zaidi ya saa mbili na maafisa wa EACC katika afisi za tume hiyo zilizoko jumba la Madison, Nairobi, Murathe alidai aliitwa kama shahidi wala sio mshukiwa wa sakata hiyo.

Lakini Jumamosi Dkt Khalwale, Muthama na Mbunge wa Mumias Mashariki Benjamini Washiali walimwonya Bw Murathe dhidi ya kuchezea jina la Dkt Ruto.

“Inasikitisha kuwa Bw Murathe anacheza na jina la Naibu Rais na kuitumia kama mwanasesere. Anapaswa kuheshimu afisi ambayo Dkt Ruto anashikilia kwa sababu ndiyo ya pili kimamlaka nchini. Ingawa ni wazi kuwa hamheshimu kama mtu binafsi hana budi kuheshimu afisi anayoshikilia kama Naibu Rais,” Bw Washiali. 

Mbunge huyo alimtaka Bw Murathe ajiuzulu wadhifa wake katika chama cha Jubilee akisema mienendo na matamshi yake yanaiharibia sifa chama hicho kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

“Bw Murathe asipojiuzulu aondolewe kwa nguvu. Chama tawala chenye wajumbe wenye katika mabunge yote hakipasi kusimamiwa na naibu mwenyekiti mfisadi,” Bw Washiali akaeleza.

Dkt Khalwale alipuuzilia mbali kauli ya Murathe kwamba yeye na Muthama wakife mbele ya EACC akisema hawajahitajika kufanya hivyo.

“Atuambie anataka tujitetee kuhusu nini katika EACC kwa sababu sisi sio kama yeye aliyeitwa kujitetea baada ya kutajwa katika sakata ya Kemsa. Hatuna makosa ya kujitetea kwayo,” akasema.

Hata hivyo, Dkt Khalwale alisema wako tayari kufika mbele ya tume hiyo kama mashahidi endapo wataitwa.