Habari

Wandani wa Ruto waingia mitini

February 16th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

AMRI ya Rais Uhuru Kenyatta kwa wanasiasa wa ‘Tangatanga’ katika eneo la Mlima Kenya kukoma kufanya siasa, sasa inaonekana kuwatia hofu baadhi yao, ambapo wameanza kususia hafla za Naibu Rais William Ruto.

Hilo lilidhihirika mnamo Ijumaa katika Kaunti ya Nyeri, wabunge wengi ambao wamekuwa wakimpigia debe Dkt Ruto kuwania urais mnamo 2022, walipokosa kuhudhuria hafla moja ya kuchangisha pesa.

Ni wabunge wanne tu ambao waliandamana na Dkt Ruto kwenye hafla hiyo iliyofanyika katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Giakanja.

Wabunge waliokuwepo kwenye hafla hiyo ni Bi Rahab Mukami (Nyeri), Rigathi Gachagua (Mathira), Anthony Kiai (Mukurwe-ini) na George Murugara (Tharaka).

Viongozi wengine wa kisiasa waliokuwepo ni Naibu Spika wa bunge la kaunti hiyo, Bw Samuel Kariuki na diwani wa wadi ya Chinga, Bw Kiruga Thuku.

Hali ilikuwa hivyo Jumamosi katika Kaunti ya Kericho, wakati wa kutawazwa kwa Askofu Alfred Rotich wa Kanisa Katoliki Jimbo la Kericho, ambapo ni mbunge Kimani Ichungw’a (Kikuyu) pekee kutoka eneo la Mima Kenya ambaye alikuwepo.

Dkt Ruto na kinara wa chama cha ANC, Bw Musalia Mudavadi walikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria.

Katika hafla ya Nyeri, kukosekana kwa aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Bw Mwangi Kiunjuri, ambaye anatoka katika kaunti hiyo, licha ya makazi yake kuwa katika Kaunti ya Laikipia, pia kumezua maswali.

Hali hiyo ni kinyume na hafla za kawaida za Dkt Ruto, ambapo huwa anaandamana na wabunge wengi wa kundi hilo, huku wakimpigia debe kwa kusisitiza kuwa eneo hilo litamuunga mkono kwenye azma yake ya urais ya mwaka wa 2022.

Miongoni mwa wabunge hao ni Ndindi Nyoro (Kikuyu), Moses Kuria (Gatundu Kusini), Alice Wahome (Kandara), Faith Gitau (Nyandarua) kati ya wengine.

Kukosekana kwao kumezua maswali kuhusu ikiwa hatimaye ‘wamekunja mkia’ na kuzingatia onyo la Rais Kenyatta kukoma kuendesha siasa.

Ingawa baadhi yao wanasema kuwa walikuwa katika shughuli tofauti katika maeneo yao, hilo linaonekana kuwatia hofu, hasa baada yao kuzuiwa kuhudhuria hafla za Rais Kenyatta kwenye ziara alizofanya Januari katika eneo hilo.

“Sisi ni viongozi tuliochaguliwa katika maeneo yetu, ambapo ni lazima tuwatengee muda pia. Dkt Ruto ni kiongozi aliyechaguliwa kama sisi, ambapo pia ana majukumu yake binafsi. Wakati mwingine ratiba zetu huwa zinakwaruzana,” akasema Bw Nyoro.

Kwenye ziara hizo, Rais Kenyatta aliwaonya vikali viongozi hao, akisema kuwa wamekuwa wakitumia muda wao kupiga kelele bila kutoa suluhisho zozote kwa changamoto zinazowakumba wananchi.

Wabunge hao walijipata pabaya katika kaunti za Nakuru, Nyandarua na Kirinyaga, kwani walizuiwa kuingia kuingia katika hafla za Rais Kenyatta, wakisingiziwa kumkosea heshima kwa kuendeleza kampeni za 2022.

Baadhi yao wamekuwa wakiwalaumu Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i na Katibu wa Wizara, Dkt Karanja Kibicho kwa masaibu yao.

Kwenye ziara hiyo, Rais Kenyatta alieleza ghadhabu yake kwa “kusalitiwa” na viongozi ambao alikuwa akiwatuma kuwahudumia wananchi.

“Sasa nitakuwa nikikagua miradi inayoendelea binafsi bila kumtuma yeyote. Wale wanaoendelea kupiga kelele wafahamu kiboko chao chaja,” akasema.