NA SHABAN MAKOKHA
WASHIRIKA wa Rais William Ruto kutoka Kaunti ya Kakamega wamekosoa uteuzi wake wa Mawaziri Wasaidizi (CASs), wakidai amewapuuza wandani wake muhimu na kuwateua wanasiasa wapya ambao hawakumsaidia katika kampeni.
Mnamo Alhamisi, Rais Ruto aliwateua washirika wake 50 kuwa CASs ili kupigwa msasa na Bunge la Kitaifa, hali ambayo imeibua ukosoaji mkali kutoka mirengo tofauti ya kisiasa.
Baadhi ya Wakenya wamemkosoa Rais Ruto kwa kuwateua ‘wanasiasa waliokataliwa’, kuwajumuisha watu waliokuwa katika upinzani wakati wa kampeni za 2022 na kuwateuwa CASs wengi kupita kiasi wakati nchi inakabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi.
Wakenya wengi wamezua maswali kuhusu sababu za utawala wa Kenya Kwanza kuongeza idadi ya CASs wakati Kenya inazongwa na madeni makubwa ya kimataifa na fedha nyingi inazotumia katika kulipia mishahara ya wafanyakazi.
Nao wafuasi wa aliyekuwa Waziri wa Michezo, Rashid Echesa walimrai Rais Ruto kumpa kazi katika serikali yake.
Subscribe our newsletter to stay updated