Habari Mseto

Wandani wa Ruto wasema wanaompinga wamelipwa na Moi

November 21st, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

WANDANI wa naibu wa Rais William Ruto wamezidi kujitokeza kumtetea kufuatia mavamizi aliyopokea kutoka kwa wabunge watatu wa bonde la ufa, wote wakimlaumu seneta wa Baringo Gideon Moi kuwa kiini.

Wa hivi punde zaidi kumtetea Bw Ruto ni mbunge wa Kapseret Oscar Sudi na seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, ambao wote wamedai kuwa watatu hao walilipwa na Bw Moi kumchafulia jina naibu wa Rais.

Wabunge Alfred Keter wa Nandi Hills, Joshua Kuttuny wa Cherangany na Silas Tiren wa Moiben wiki iliyopita walitoa madai makali ya kumhusisha Bw Ruto na sakata za mahindi na mbolea, wakiitisha uchunguzi dhidi yake.

Watatu hao walidai kuwa Bw Ruto pamoja na ofisi yake ndio wamesababisha matatizo wanayokumbana nayo wakulima wa eneo la bonde la ufa.

Lakini Jumanne, Bw Cheruiyot alijitokeza kumtetea Bw Ruto, akisema wabunge hao hawakuwa wakiwatetea wananchi, bali maslahi yao.

“Hawa ni watu ambao wamelipwa na wakulima hawafai kudhani kuwa wanazungumza kwa niaba yao, wako na ajenda fiche. Katika vikao vyao vyote huwa wanamlenga naibu wa Rais ili kumchafulia jina,” akasema seneta huyo wa Kericho.

Bw Cheruiyot alisema kuwa kila kukitokea tatizo ndani ya serikali, wapinzani hao wa Bw Ruto wamekuwa wakitafuta sababu ya kumhusisha Bw Ruto ili kumharibia jina.

Jumatatu, Bw Sudi naye alidai kuwa ni Bw Moi ambaye anawatumia watatu hao ili kummalizia umaarufu Bw Ruto wakati mbio za ikulu 2022 zikishika kasi.

“Biashara ni kumpaka William Ruto uchafu ili asifike 2022. Ikiwa mnaongea ukweli mjipange muende kwa EACC mpige ripoti.

“Wanafanya kazi ya ‘usher’ huko Kabarak kisha wakilipwa wanajifanya wanawatetea wakulima. Badala mkuje mseme nyinyi ni wapinzani wa Ruto mnakuja kusema mnatetea wakulima,” akasema Bw Sudi.

Alishangaa sababu ya naibu wa Rais kuhusishwa na takriban kila sakata inayotokea.

“Kwani huyu William Ruto ni mwizi kiasi gani, kwani amewaibia nini? Huyo mgombeaji kama ni Gideon Moi ndio mnatakia awe Rais, hamna bahati,” akasema.