Habari Mseto

Wandani wa Ruto wathubutu kusema 'tutapigania Miguna kurejea nchini'

July 10th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

VITA vya ndani kwa ndani katika serikali ya Jubilee vinazidi huku mpasuko baina ya kambi zinazounga mkono Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto ukizidi kuwa mkubwa.

Wakati mkurugenzi wa masuala ya kidijitali Ikulu, Dennis Itumbi alifikishwa kortini Jumatano, baadhi ya wabunge wa kundi la Tangatanga walijitokeza kuungana naye, wakilaumu kuwa wamekuwa wakiwindwa kutokana na uamuzi wao wa kumuunga Dkt Ruto mkono.

Hata hivyo, ni matamshi ya mbunge wa Kapseret Oscar Sudi ndiyo yalikuja bila kutarajiwa, akikiri kuwa serikali haikumtendea haki wakili Miguna Miguna alipotimuliwa mwaka 2018, na kudai kuwa atawataka Wakenya kupigania wakili huyo arejeshwe nchini.

Bw Sudi amesema kukamatwa kwa Bw Itumbi hakuna tofauti na jinsi wakili Miguna alihangaishwa kabla ya kutimuliwa.

“Tunataka kuwaambia tunajua zaidi na tutasimama imara, mchunge watu wangapi, mpangie wangapi ama mshike watu wangapi, hatutasimamisha maono ambayo tuko nayo,” akasema mbunge huyo, mfuasi sugu wa Naibu Rais.

Aliendelea kusema “Hii haina tofauti na jinsi walizungusha Miguna Miguna. Na ningependa kuwaomba marafiki zangu na Wakenya, baada ya hii tuanze kupigania kurejeshwa kwa Miguna nyumbani. Haya ni maneno ya enzi za Kanu ambazo zilipitwa na wakati. Hatutishwi, tuko Kenya hii na sisi sio maskuota.”

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa kiongozi kutoka mrengo wa Jubilee kukiri kuwa Bw Miguna alitimuliwa nchini kinyume na sheria, licha ya serikali kukataa kabisa kumpa pasipoti yake ya Kenya.

Kwa upande mwingine, ni matamshi ambayo yameonyesha jinsi kumeibuka msambaratiko mkubwa katika chama hicho tawala, ambao umezidi siku za majuzi.