Wandani wa Uhuru wajaa hofu katika serikali ya Ruto

Wandani wa Uhuru wajaa hofu katika serikali ya Ruto

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto amejipata katika njiapanda kufanya kazi na wakuu wa taasisi muhimu za serikali aliodai kwamba walitumiwa na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta, kumhangaisha.

Miongoni mwa maafisa hao ni Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai, Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) George Kinoti, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Alexander Muteshi na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak.

Wengine ni Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na Naibu Mkuu wa Majeshi Francis Ogolla.

Miongoni mwa maafisa hawa, ni Mabw Kinoti na Muteshi pekee ambao Dkt Ruto anaweza kutumia ushawishi wake kuhakikisha kuwa wanatimuliwa mara moja.

Wengine wanalindwa na Katiba na haitakuwa rahisi kwa Rais Ruto kuwafuta kazi bila kupata idhini ya Bunge.

Wakati wa kampeni za kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, Dkt Ruto na wandani wake waliwashutumu Mabw Mutyambai na Kinoti kwa kutumiwa na serikali kuhangaisha wanasiasa wa muungano wake wa Kenya Kwanza kwa kisingizio cha kupambana na ufisadi.

Akiongea katika uwanja wa Kasarani alipoongoza hafla ya uzinduzi wa manifesto ya Kenya Kwanza, Dkt Ruto aliahidi kuwachunguza wawili hao kwa nia ya kuwaadhibu.

“Katika serikali yetu ya Kenya Kwanza, ambayo tutaunda Mungu akipenda baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, Idara ya Polisi itakuwa huru. Haitatumiwa kuwaandama wanasiasa kwa njia isiyo halali ilivyo sasa chini ya serikali hii ya handisheki,” akasema.

“Nataka ifahamike kuwa wale ambao wamekuwa wakitumiwa kuendesha shughuli za kisiasa watachunguzwa na kufutwa kazi,” akaongeza.

Aidha, mnamo Julai 28, akihutubu katika uwanja wa Kapkatet, kaunti ya Kericho Dkt Ruto alimwonya Bw Kinoti dhidi ya kuingilia utendakazi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

“Umefeli kama DCI. Hatutaki utatize tena uchaguzi huu. Koma kabisa kutukasirisha na uache IEBC ifanye kazi yake. Kazi yako ni kupeleleza jinai na haujafanya chochote kando na kuwaandama wanasiasa bila sababu maalum. Subiri Agosti na utaenda nyumbani,” Dkt Ruto akafoka.

Kiongozi huyo na wandani wake walikasirishwa na hatua ya maafisa wa DCI kuwakamata raia watatu wa kigeni katika uwanja wa JKIA, Nairobi wakiwa na bidhaa ambazo zilinuiwa kutumika na IEBC katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2022.

Aidha, mwaka 2021, maafisa wa DCI walimkamata Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusiana na tuhuma za wizi wa Sh7.5 bilioni, pesa za umma.

Kesi hiyo ingali mahakamani.Rais Ruto sasa ana mamlaka ya kushawishi kufutwa kazi kwa Bw Kinoti.

Bw Mutyambai, naye, analindwa kikatiba na hawezi kufutwa kabla ya muda wake wa kuhudumu kukamilika.

Lakini duru zasema kuwa Inspekta Jenerali huyo anastaafu mnamo Aprili 2023 atakapotimu umri wa miaka 60.

Jana Ijumaa, Rais Ruto amekabidhi Bw Mutyambai mamlaka ya kusimamia bajeti ya Polisi.

Dkt Ruto pia hawezi kuwafuta kazi Mabw Haji (DPP) na Mbarak ambao afisi zao zinalindwa kikatiba.

Hata hivyo, mwandani wa Rais anaweza kuwasilisha hoja katika bunge la kitaifa kwa ajili ya kuwaondoa wawili hao.

Wawili hao wamekuwa wakiwachunguza wandani wa Dkt Ruto kuhusiana na tuhuma za ufisadi mauji.

Kwa upande wake Bw Muteshi hana bahati kwa sababu anaweza kupigwa kalamu wakati wowote.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2021, Mkurugenzi huyo wa idara ya uhamiaji alitumiwa na Waziri wa Usalama Fred Matiang’i kufurusha raia wa Uturuki Harun Aydin.

Aydin alikuwa miogoni mwa wageni waliohudhuria sherehe ya kuapishwa kwa Dkt Ruto Jumanne.

Raia huyo wa Uturuki ni mwandani wa Rais Ruto na Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, alituhumiwa kuwa nchini kinyume cha sheria na kushiriki ulanguzi wa kifedha.

Luteni Ogolla, ambaye anastaafu 2024, amekuwa akishutumiwa na wandani wa Dkt Ruto kwa kushiriki njama ya kumlazimisha Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati kumtangaza Raila Odinga kama mshindi wa urais.

Ogolla alikuwa miongoni mwa wanachama wa Baraza la Kitaifa la Ushauri kuhusu Usalama (NSAC) walienda katika kituo cha kitaifa cha kujumuisha kura za urais, Bomas of Kenya, usiku wa kuamkia Agosti 15.

  • Tags

You can share this post!

Miili 440 yapatikana kwenye kaburi Ukraine

Walimu wataka serikali iwajumuishe katika jopokazi...

T L