Wandayi awaomba waajiri kuwapa wafanyakazi ruhusa ya kushiriki maandamano Jumatatu, Machi 20, 2023

Wandayi awaomba waajiri kuwapa wafanyakazi ruhusa ya kushiriki maandamano Jumatatu, Machi 20, 2023

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa wachache katika Bunge la  Kitaifa Opiyo Wandayi sasa anawaomba waajiri kote nchini waachilie wafanyakazi wao Jumatatu ili wapate nafasi ya kushiriki maandamano.

Akiwahutubia wanahabari mnamo Alhamisi katika majengo ya bunge, Nairobi, Bw Wandayi alisema wanafanyakazi wote isipokuwa wanahabari wanafaa “kushiriki katika maandamano hayo kwa sababu kiongozi wa Azimio Raila Odinga ametangaza Jumatatu kama siku ya mapumziko.”

“Kwa kuwa Jumatatu imetangazwa kuwa siku ya mapumziko, waajiri wote isipokuwa wamiliki wa vyombo vya habari wanapaswa kuwaachiliwa wafanyakazi wao washiriki maandamano ya kutetea kile ambacho ni haki yao. Ni matumaini yetu kwamba waajiri wote watatii wito wetu,” Bw Wandayi ambaye ni Mbunge wa Ugunja akasema.

Kwa upande wake, Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna alisema kuwa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya umelazimika kuwashauri Wakenya kushiriki maandamano baada ya serikali kukataa kutekelezwa matakwa yao, ikiwemo kupunguza gharama ya maisha.

“Kuna matakwa fulani ambayo tuliwasilisha ili serikali hii ishughulikie, mojawapo ikiwa ni kupanda kwa bei ya unga, kurejeshwa kwa ruzuku kwa bei ya bidhaa za msingi, kukataa kufungua sava ya IEBC, na kushuka kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni,” Katibu huyo mkuu wa ODM akaeleza.

Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna akihutubia wanahabari mnamo Alhamisi. PICHA | CHARLES WASONGA

Wengine waliohutubia kikao hicho cha wanahabari ni kiongozi wa wachache katika seneti Stewart Madzayo, Seneta wa Makueni Daniel Maanzo, mbunge wa Nyando Jared Okello, Mishi Mboko miongoni mwa wengine.

  • Tags

You can share this post!

Wabunge wa Kenya Kwanza wadai maandamano ya Raila ni sawa...

Idadi ya watu waliouawa na kimbunga Freddy, Malawi imefika...

T L