WANDERI KAMAU: Amerika inavyotumia unafiki kuendeleza uporaji

WANDERI KAMAU: Amerika inavyotumia unafiki kuendeleza uporaji

Na WANDERI KAMAU

UKOLONI-mamboleo haujikiti kwenye siasa pekee. Vilevile, upo kwenye mawanda ya kiuchumi, kidini, kitamaduni na kijamii.

Kinyume ilivyokuwa katika miaka ya hamsini, sitini na sabini, mataifa yenye nguvu kwa sasa yamebuni mbinu za kijanja kuzipora nchi maskini kwa kisingizio cha “kuzisaidia kurejesha uthabiti wa kisiasa.”

Hiyo ndiyo simulizi kuu inayoandama hatua ya Amerika kuivamia Afghanistan mnamo 2001 na baadaye kuyaondoa majeshi yake kighafla mwaka huu.

Alipoyatuma majeshi hayo nchini humo, aliyekuwa rais wa Amerika wakati huo, George Bush, alisema msukumo huo ulitokana na shambulio la Septemba 11, 2001, lililofanywa na kundi la Al-Qaeda katika miji ya New York na Washington DC.

Kwenye shambulio hilo la kigaidi, zaidi ya watu 3,000 walipoteza maisha yao.Kwa ghadhabu, Bush alifuata nyayo za babake, marehemu George Herbet Bush, ambapo alivamia nchi ya Kuwait katika miaka ya tisini, kwenye uvamizi uliofahamika kama ‘Vita vya Ghuba’.

Kando na Afghanistan, Bush pia alivamia Iraq na kumwondoa mamlakani aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo, Saddam Hussein, kwa kisingizio cha kutengeneza silaha za kinuklia.

Cha kusikitisha ni kuwa katika vamizi hizo zote, Amerika huwa inayaacha mataifa hayo yakiwa kama vigae.Baada ya kifo cha Saddam, Iraq haijawahi kushuhudia uthabiti wa kisiasa na kiuchumi uliokuwepo awali.

Nchini Afghanistan, hali ni tete. Raia wanafanya kila wawezalo kuondoka humo kwa njia yoyote ile.

Wengine wamenaswa wakining’inia kwenye ndege—yote kwa kuhofia utawala wa wanamgambo wa kundi la Taliban.Hayo hayatoshi.Nchi ya Libya inapitia mvurugiko wa kiutawala unaoshuhudiwa Iraq na Afghanistan.

Baada ya serikali ya aliyekuwa rais wa Amerika, Barack Obama, kuivamia kwa kisingizio cha kumwondoa mamlakani Muammar Gaddafi, taifa hilo limegeuka kuwa uwanja wa vita na mahangaiko ya kila namna.Kwa sasa, haijulikani kuhusu yule anayefaidika kutokana na mafuta yaliyo katika nchi za Libya na Iraq.

Vivyo hivyo, haijulikani kuhusu yule atakayefaidika kutokana na raslimali asilia zenye thamani ya mamilioni ya pesa zilizo Afghanistan.Maswali yanayoibuka ni: Mbona Amerika na washirika wake wanaihadaa dunia kwamba wanakabili ugaidi ilhali wanazipora nchi maskini? Mbona dunia imenyamazia unafiki huu wa Amerika?

Ukweli ni kuwa, lazima dunia nzima isimame kidete kukabili propaganda za uwongo ambazo zimekuwa zikienezwa na Amerika, ilhali imekuwa ikitumia uwezo wake wa kijeshi kuendeleza uporaji na ukoloni-mamboleo wa kiuchumi.

akamau@ke.nationmedia.com

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: Tuwasitiri na tuwapende wakimbizi wa...

Mwanasheria Mkuu kukata rufaa ya BBI katika Mahakama ya Juu