WANDERI KAMAU: Hukumu ya Sarkozy isaidie Waafrika kufunguka macho

WANDERI KAMAU: Hukumu ya Sarkozy isaidie Waafrika kufunguka macho

Na WANDERI KAMAU

MOJAWAPO ya nguzo zilizozipa utambulisho jamii na tawala za kale, ni aina ya adhabu zilizotolewa kwa wale waliokiuka kanuni na taratibu zilizowekwa.

Jamii hizo zilikuwa na taratibu maalum za kumwadhibu yeyote aliyekisiwa kukiuka sheria zilizowekwa, ili kuendeleza maadili na uwajibikaji miongoni mwa wanajamii.

Ingawa hukumu ya kifo imekuwa ikizua hisia na midahalo katika majukwaa mbalimbali duniani, haikuanzia majuzi, bali imekuwepo kwa muda mrefu.

Miongoni mwa Wamisri, watu waliokabiliwa na hukumu kali zaidi ni wezi ama waporaji.

Kulingana na taratibu za jamii za jadi nchini humo, wezi waliwekwa kwenye kapu moja na wauaji.

Wezi walionekana kama watu wakorofi, wenye tamaa, wasaliti na waliokuwa tayari kufanya lolote kujitajirisha, bila kujali mustakabali wa jamii hizo. Walionekana kama wakosa ubinadamu.

Kutokana na fasiri hizo, walichukuliwa kama maadui wakuu wa jamii. Ili kuwaondoa kabisa, miongoni mwa adhabu zilizotolewa kwa wezi ni kifo. Hawakuhurumiwa hata kidogo.

Katika falme ya Misri, wafalme walikuwa wakiagiza wale waliopatikana na hatia za wizi kurushiwa mbwa mwitu ama simba maalum waliokuwa wakifugwa kuwala watu hao.

Chini ya taratibu hizo, watu wengi walijaribu kujiepusha na makosa yoyote yaliyohusiana na wizi.

Kando na Misri, mataifa mbalimbali yalikumbatia adhabu hizo, miongoni mwayo yakiwa China na Japan.

Nchi kadhaa za Ulaya pia zimeorodhesha ufisadi kuwa miongoni mwa makosa yenye adhabu kali zaidi.

Hilo lilidhihirishwa na adhabu iliyotolewa dhidi ya aliyekuwa rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, Jumatatu, baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi.

Kwenye hukumu ya kihistoria iliyotolewa na mahakama, Sarkozy alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani kwa kosa la kujaribu kupata maelezo kutoka kwa hakimu kuhusu kesi iliyokuwa ikiendelea dhidi yake.

Tangu Jumatatu, hukumu hiyo imezua hisia mseto katika sehemu mbalimbali duniani, baadhi wakiisifu huku wengine wakiilaumu mahakama kwa “maonevu” dhidi ya kiongozi huyo.

Hata hivyo, Wafaransa wengi wanalichukulia hilo kama jambo la kawaida, kwani wafisadi huwa hawahurumiwi.

Swali ni: Waafrika watajifunza lolote kutoka kwa hukumu hiyo? Ni taifa lipi la Afrika, Kenya ikiwemo, linaloweza kumhukumu rais kwa tuhuma za ufisadi?

Kinaya ni kuwa, Waafrika huwa wanawakweza na ‘kuwaabudu’ wafisadi badala ya kuwakemea. Huwa wanaonekana kama ‘mashujaa’, hasa miongoni mwa jamii wanakotoka. Wengine hata huchaguliwa kama viongozi! Kinaya!

Ni wakati Waafrika wafunguke macho, na kujua kuwa kwa kuwachagua viongozi kama hao, wanajisaliti wao wenyewe.

akamau@ke.nationmedia.com

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Wagombeaji wa kiume wazuiwe kuwadhalilisha...

KINYUA BIN KING’ORI: Raia wasipotoshwe na siasa za...