WANDERI KAMAU: Jamii zirejelee misingi ya malezi bora kuzuia mivutano

WANDERI KAMAU: Jamii zirejelee misingi ya malezi bora kuzuia mivutano

Na WANDERI KAMAU

KIAFRIKA, wazazi huwa na baraka kubwa kwa wanao na tangu utotoni mwetu, tumefunzwa kwamba wazazi wetu huwa kama ‘miungu’ wetu wa pili hapa duniani.?

Bila shaka, ingawa mafunzo hayo kwa kawaida huwa yanalenga kulainisha mienendo ya watoto wanapokua, uhalisia wake humdhihirikia mtoto ukubwani mwake hasa anapoanza kuwajibikia majukumu mbalimbali ya ulezi kama mzazi.

Huwa inamdhihirikia kuwa ulezi si jambo rahisi anapoanza kuitishwa mahitaji kama karo ya shule, vitabu, nguo na chakula.? Kwa kufahamu ugumu ambao walezi wetu walipitia ili kutufikisha tulipo, jambo la muhimu maishani mwetu ni kuwashukuru.

Ijapokuwa haijaandikwa popote pale kuwa sharti “shukrani” hizo ziwe ni jambo la lazima, ni muhimu kwa kila mmoja kuangalia nyuma na kutathmini kwa kina michango ambayo walezi wetu walitoa utotoni mwetu.? Hilo pekee linapaswa kutuzindua kimawazo kuwa tuna jukumu la kuwapa shukrani walezi hao, japo kulingana na uwezo mtu alio nao.

Hata hivyo, huwezi kumpa mtu Sh1,000 ilhali uwezo wako ni Sh500 pekee.? Vivyo hivyo, huwezi kumnunulia mtu gari au nyumba ilhali kamwe huna uwezo huo. Kunapaswa kuwa na hali ya maelewana kati ya pande zote mbili—wazazi (walezi) na wanao.

Urejeleo huu unafuatia visa ambapo baadhi ya wazazi nchini wamekuwa wakiwalaumu au hata kuwashtaki wanao mahakamani kwa kuwatelekeza. Hivi ni visa vya aina yake, maanake ni nadra sana mzazi kumshtaki mwanawe mahakamani, akiitaka kuifanya lazima awe akimsaidia.

Kimsingi, huenda kuna mivutano ya ndani ya kifamilia iliyofichika, kwani si kawaida kwa mzazi kuchukua uamuzi mzito kama huo bila kujali athari zake—hasa mustakabali wa mahusiano kati yake na mwanawe au wanao.? Hata hivyo, ni matukio yanayopaswa kuzua mdahalo kuhusu mahusiano yaliyopo baina ya watoto na wazazi wao, hasa wanapoenda mijini baada ya kupata ajira.

Binafsi, siegemei upande wowote, kwani sina ufahamu wa kina kuhusu aina ya mahusiano ambayo huwepo kati ya wazazi na wanao kuanzia utotoni hadi ukubwani mwao.Kwanza, kuna wazazi (hasa wanaume), ambao wamekuwa wakilaumiwa na wanao kwa kuepuka majukumu ya ulezi na kujitokeza tu wakati watoto wao wanafaulu maishani.

Pili, kuna wazazi ambao huwatesa wanao wa kambo hasa katika hali ambapo mwanaume au mwanamke anaoa au kuolewa akiwa na watoto kutoka mahusiano au ndoa ya awali.? Katika hali kama hizo, yatakuwa makosa makubwa kwa jamii kuwahukumu watoto bila kufahamu ukweli.

Vile vile, kuna wazazi wenye mazoea ya kuwa na matarajio makubwa sana kwa watoto wao bila kufahamu changamoto za kimaisha wanazopitia.? Ili kuepuka haya, ni lazima jamii ikuze mazingira ya maelewano, ushirikiano na umoja baina ya wazazi na wanao kama ilivyokuwa zamani.

You can share this post!

TAHARIRI: Hawakustahili kufa namna ile katika ajali ya basi...

Raila asuka njama ya kumzima Ruto Pwani

T L