WANDERI KAMAU: Kenya itangaze msimamo thabiti kuhusu mashoga

WANDERI KAMAU: Kenya itangaze msimamo thabiti kuhusu mashoga

NA WANDERI KAMAU

DUNIA inapoendelea kushuhudia mabadiliko mengi, hasa katika masuala ya kitamaduni, baadhi ya mabadiliko hayo ibuka yamezua mgongano mkubwa wa kitamaduni miongoni mwa jamii za Kiafrika.

Kama kawaida, kuna makundi yanayoshikilia kuwa mchipuko huo wa tamaduni ibuka unalenga kuzipotosha jamii, kwa kuleta mitindo ya kimaisha ambayo kamwe hailingani na Uafrika halisi.

Vivyo hivyo, kuna makundi yenye mitazamo kinzani—yanayosema kuwa lazima Afrika iwe tayari kukumbatia tamaduni hizo mpya “ili kuwiana na dunia ya kisasa.”

Je, kati ya makundi hayo mawili kinzani, ni nani mkweli na ni yupi anayeipotosha jamii?

Miongoni mwa “mitindo mipya ya kimaisha” ambayo imeibuka ni utata kuhusu nafasi ya watu au ndoa za jinsia moja katika jamii za Kiafrika.

Mwanzoni, hili ni suala lililoonekana kuwa la jamii za Magharibi na ambalo kamwe halingetokea Afrika hata kidogo.

Lilionekana “kumilikiwa” na Wazungu, hivyo ingekuwa vigumu sana kwake kufika Afrika, licha ya mwingiliano mkubwa ambao huwepo kati ya Wazungu na Waafrika.

Hata hivyo, ni wazi kuwa mtindo huu umepanuka na kusambaa kote kote duniani—hata Afrika kwenyewe!

Awali, mashoga wengi walikuwa wakiogopa kujitokeza wazi kutangaza hali zao kwa hofu kuwa huenda wakageukwa na kutengwa na jamii.

Wengi waliishi maisha ya kisiri, wakifanya lolote wawezalo kutogundulika.

Lakini hali imebadilika. Katika nchi kama Amerika na Uingereza, tayari mabunge ya mataifa hayo yamepitisha sheria za kuwatambua watu hao na kulinda haki zao.

Baadhi ya nchi za Afrika kama Afrika Kusini na Botswana pia zimebuni sheria zinazowatambua watu hao.

Hapa Kenya, bado kuna hali ya mivutano ya kichinichini baina ya serikali, jamii na taasisi husika kwa jumla, ikiwa watu hao wanapaswa kutambuliwa kisheria au la.

Kinaya ni kuwa, wakati mivutano hiyo inaendelea, baadhi ya Wakenya wamejitokeza wazi na kutangaza kuwa mashoga.

Miongoni mwao ni marehemu Binyavanga Wainaina, aliyekuwa miongoni mwa waandishi maarufu sana nchini.

Swali linaloibuka ni: Jamii inapaswa kuwakubali watu hao? Nafasi yao ni ipi katika jamii inayoshikilia mitindo ya kimaisha ya kikale?

Bila shaka hayo ni maswali magumu, ambayo hata Rais William Ruto mwenyewe ameonekana kuyakwepa licha ya kusisitiza kuwa Kenya ni nchi inayozingatia tamaduni za Kiafrika.

Hata hivyo, wakati umefika tukubali kuwa watu hao wapo miongoni mwetu, ambapo lazima tubuni mazingira yatakayowawezesha kuishi maisha yao ya kawaida bila hofu yoyote.

Ingawa hili halilengi kuishinikiza jamii kukumbatia mtindo huo wa kimaisha, inafika wakati ambapo hatuwezi kukana uhalisia ulio nasi katika mazingira tunayokaa.

La muhimu kwa sasa ni Bunge la Kitaifa kubuni sheria itakayowatambua rasmi, japo kwa kuweka masharti makali kwa yeyote kutambulika na kukubalika kisheria.

Hivyo ndivyo tutaondoa utata na migongano iliyopo kuhusu nafasi yao katika jamii ya sasa.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Mukuru wahimizwa wasafishe mazingira visa vya...

Serikali ichunguze ‘shule bandia’ zinazodaiwa...

T L