WANDERI KAMAU: Korti zetu ziige mataifa mengine kuboresha utendakazi

WANDERI KAMAU: Korti zetu ziige mataifa mengine kuboresha utendakazi

TANGU uhuru, Idara ya Mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha maamuzi ya baadhi ya kesi zinazowasilishwa kwake, kwa miaka mingi bila sababu zifaazo.

Baadhi ya kesi zimedaiwa kuchukua hata zaidi ya miaka 10 kutokana na ukosefu wa utaratibu maalum kuhusu uendeshaji wake.

Tatizo jingine ni mkinzano wa maamuzi yanayotolewa na mahakama kuhusu kesi.Kwa mfano, nchini Amerika ilichukua chini ya mwaka mmoja kwa korti kumhukumu polisi Derek Chauvin, aliyekuwa mshtakiwa mkuu katika mauaji ya raia mweusi George Floyd mwaka jana.

Baada ya uchunguzi mkali na ufuatiliaji wa kina kuhusu ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, ilidhihirika wazi kuwa Chauvin ndiye alishiriki mauaji hayo.

Alihukumiwa miaka 22 gerezani.Nchini Korea Kusini, aliyekuwa rais Park Geun-hye alitupwa jela kwa miaka 24, baada ya mahakama kumpata na hatia ya ufisadi na kutumia mamlaka vibaya.

Hukumu hiyo ilitolewa 2018 baada ya uchunguzi wa kina, unaodaiwa hata kuendeshwa kwa njia za kisayansi na kiteknolojia ili kuthibitisha mashtaka.

Nchini Afrika Kusini, rais wa zamani Jacob Zuma yuko jela baada ya korti kuagiza akamatwe.Hili ni baada ya Mahakama ya Kikatiba kumtupa miezi 15 korokoroni kwa kukosa kuhudhuria vikao vya kusikilizwa kwa kesi yake ya ufisadi.

Kama hilo halitoshi, kesi za watu wanaotuhumiwa kushiriki mauaji ya Wayahudi, wakati wa utawala wa Adolf Hitler nchini Ujerumani miaka ya arobaini, bado zinaendelea kusikilizwa hadi sasa.

Mifano hiyo inaibua uhalisia uliopo kuhusu michakato ya kisheria katika nchi nyingine.Michakato hiyo huzingatia haki, huharakisha kesi, huendeshwa kwa njia ya kisasa na haitupilii mbali kesi ovyo.

Kinyume na mataifa hayo, taswira ya kisheria ni tofauti sana hapa nchini Kenya.Kijumla, ni tofauti katika hali zote zilizotajwa hapo juu.

Katika mahakama zetu, hutashangaa kusikia uamuzi tofauti ukitolewa na mahakama mbalimbali, kuhusu kesi moja iliyowasilishwa kwazo.

Ni katika mahakama zizo hizo utasikia mshtakiwa “akiachiliwa huru” baada ya kufungwa kwa hata zaidi ya miaka kumi; kwa kisingizio cha “ukosefu wa ushahidi.”

Maamuzi hayo yanaibua hofu na maswali kuhusu taratibu zinazofuatwa na mahakama zetu katika utoaji wa maamuzi yake. Ni wakati ziige taratibu za kisheria katika nchi nyingine ili kulainisha utendakazi wake.

akamau@ke.nationmedia.com

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: ‘Mashujaa’ wanaoibia umma wafungwe jela

Ushuru wa miraa, muguka kupanda