WANDERI KAMAU: Maombi yamedhihirisha tena unafiki wetu kama jamii

WANDERI KAMAU: Maombi yamedhihirisha tena unafiki wetu kama jamii

NA WANDERI KAMAU

PENGINE unafiki wetu kama binadamu ndio huwa unamfanya Mungu kutukasirikia na wakati mwingine kutuadhibu.

Mwanadamu amegeuka kuwa kiumbe mwenye hadaa na tamaa iliyopita mipaka.

Mfano huo unaashiriwa na Hafla ya Kitaifa ya Maombi ambayo ilifanyika Alhamisi jijini Nairobi iliyoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na viongozi kadhaa wa kidini.

Kwenye hafla hiyo, viongozi wa kisiasa walitoa matamshi matamu ya “kumshukuru” Mungu kwa amani ambayo ameijaalia Kenya kwa muda mrefu.

Naibu Rais William Ruto, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi, Jaji Mkuu Martha Koome, mwanasiasa Martha Karua kati ya wengine walitoa hotuba zao tamu kwa kurejelea Biblia na vitabu vingine vitakatifu. Kauli kama hiyo ndiyo aliyotoa Rais Kenyatta.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa licha ya matamshi na hotuba hizo tamu kutoka kwa viongozi hao, mwelekeo wa Kenya katika karibu kila nyanja unaendelea kutikisika.

Kwa mfano, serikali ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto imekuwa ikilaumiwa kwa kila aina ya maovu—kama vile ufisadi, kupanda kwa gharama ya maisha, kuongezeka kwa deni la kitaifa kati ya maovu mengine.

Ni wazi kuwa ni wakati wa utawala wa serikali ya Jubilee ambapo Kenya imeshuhudia mojawapo ya sakata kubwa zaidi za ufisadi tangu tulipojinyakulia uhuru.

Baadhi ya sakata hizo ni uporaji wa fedha katika Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), mabwawa ya Arror na Kimwarer, Eurobond (I na II) kati ya nyingine.

Maswali yanayoibuka ni: Ikizingatiwa imekuwa kawaida kwa hafla kama hizo za maombi kufanyika kila mwaka, mbona maovu hayo yamekuwa yakishuhudiwa? Mbona Rais Kenyatta na Dkt Ruto wameshindwa kusuluhisha tofauti zao za kisiasa tangu 2018? Mbona wameshindwa kutimiza ahadi nyingi walizotoa kwa Wakenya licha ya kuegemeza “utendakazi” wao kwa Mungu?

Bila shaka, hafla ya Alhamisi (na nyingine za hapo awali) inaiakisi Kenya kama jamii iliyozama katika lindi la unafiki. Ni unafiki ambao huenda Mungu akakosa kutusamehe.

Kwenye hafla ya Alhamisi, Dkt Ruto aliahidi kuzingatia amani na kukubali matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti.

Bi Karua, aliyemwakilisha mwaniaji urais wa muungano wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga, alitoa ahadi kama hiyo.

Kwa kurejelea historia na matukio ya hapo awali, baadhi ya viongozi wanaotoa ahadi hizo ndio wao hao wanaohusishwa na baadhi ya maovu yaliyotokea hapo awali.

Kwa mfano, Dkt Ruto amekuwa akihusishwa na maovu yaliyofanywa na kundi la YK’92, alilobuni marehemu Daniel Moi kumfanyia kampeni kwenye uchaguzi mkuu wa 1992.

Hali ni iyo hiyo kwa kila mwanasiasa aliyehudumu katika tawala za Mzee Jomo Kenyatta na Mzee Moi.

Uchaguzi mkuu unapoendelea kukaribia, wito wetu ni kwa wanasiasa kuzingatia na kutimiza ahadi wanazotoa, badala ya kuendeleza unafiki kama ambavyo wamekuwa wakifanya tangu jadi.

akamau@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

DOMO: Inasikitisha Omosh kashuka levo hizi!

Omanyala apata saizi yake Ujerumani

T L