WANDERI KAMAU: Mataifa ya Afrika yaungane kupata ufanisi wa kudumu

WANDERI KAMAU: Mataifa ya Afrika yaungane kupata ufanisi wa kudumu

NA WANDERI KAMAU

MATUMAINI ya Waafrika wengi yalikuwa kwamba, bara hili lingeweza kujinasua kutoka kwa msururu wa changamoto zilizoikumba, baada ya kujinyakulia uhuru kutoka kwa wakoloni miaka ya sitini.

Waafrika walikuwa wakiishi kama watumwa katika bara lao. Ilikuwa vigumu kutembea mahali popote ama kuendesha biashara bila vibali maalum kutoka kwa serikali za kikoloni.

Ilikuwa vigumu kwao kupata elimu, kucheza baadhi ya michezo, kula baadhi ya vyakula na hata kuajiriwa baadhi ya kazi, kutokana na ubaguzi mkubwa uliokuwepo dhidi yao.

Baadhi ya wakoloni waliwafananisha Waafrika na wanyama au nusu binadamu.

Ukatili huo ndio uliowafanya Waafrika kuungana na kuchukua silaha ili kuwakabili wakoloni.

Kinaya ni kwamba, licha ya mataifa mengi kuwa na matumaini makubwa kupata ufanisi wa kisiasa, kiuchumi, kijamii na kitamaduni, matumaini hayo yamegeuka ndoto isiyotimia.

Sababu ni kuwa, wakati ambapo nchi nyingi duniani zinaangazia mikakati zinazoweka kujikuza kiviwanda na kiteknolojia, mataifa mengi ya Afrika bado yanajadili kuhusu njia ambazo yatatumia kurejesha amani na uthabiti wa kisiasa.

Kwa mfano, Jumanne, Rais Uhuru Kenyatta aliwaongoza marais kadhaa wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kujadili kuhusu mkakati wa kurejesha amani DRC Congo.

Hili linafuatia mgogoro ambao umekuwepo nchini humo kwa muda mrefu, hasa kati ya majeshi ya serikali na wanamgambo wa kundi la M23.

Kikao hicho, ambacho kilifanyika katika Ikulu ya Nairobi, kiliwashirikisha marais Yoweri Museveni (Uganda), Evariste Ndayishime (Burundi), Paul Kagame (Rwanda) na Salva Kiir (Sudan Kusini).

Baada ya kikao hicho, viongozi hao walikubaliana kuhusu kubuniwa kwa kikosi cha kikanda cha kurejesha amani DRC Congo, bila kuishirikisha Rwanda.

Kwa muda mrefu, Rais Tshisekedi amekuwa akiilaumu Rwanda kwa kuunga mkono makundi ya wanamgambo kama M23 na Alliance for Democratic Forces (ADF), kutekeleza mashambulio katika himaya yake, hasa mkoa wa Kivu Kaskazini.

Kando na tofauti zilizopo kati ya DRC Congo na Rwanda, taifa hilo (DRC) pia limekuwa likitofautiana vikali na Uganda, likiilaumu serikali ya Rais Museveni kwa “kuendesha njama za kichinichini kuchukua udhibiti wa maeneo yenye utajiri wa madini.”

Bila shaka, inasikitisha kuwa wakati mataifa mengine duniani yanaungana kujadili kuhusu mikakati ya kujiimarisha kiteknolojia, mataifa ya Afrika yanaungana kujadili masuala yaliyopaswa kujadili na kusuluhisha katika miaka ya sabini, themanini na tisini.

  • Tags

You can share this post!

Watu 4 wafariki katika ajali ya ndege ya mizigo ya Urusi

Tetemeko laua watu 1,000 Afghanistan

T L