WANDERI KAMAU: Mataifa yazingatie uhuru wa kila mtu kujieleza

WANDERI KAMAU: Mataifa yazingatie uhuru wa kila mtu kujieleza

Na WANDERI KAMAU

KATIKA nchi zilizostawi kidemokrasia, raia huwa huru kutoa maoni yao kuhusu masuala tofauti bila kuogopa kutishwa kwa namna yoyote ile.

Ni uhuru ulio kwenye Katiba na taratibu za utawala wa nchi husika.

Hivyo, viongozi huwa hawana mamlaka yoyote kikatiba kuwatishia raia, wanaharakati au vyombo vya habari kueleza hisia zao kuhusu mambo yanayoendelea katika mataifa hayo.

Hali hiyo ndiyo imechangia ustawi wa demokrasia katika nchi zenye ushawishi duniani kama vile Amerika, Uingereza, Japan, Israeli, Ujerumani kati ya mengine.

Vivyo hivyo, ni uhuru huo uliochangia pakubwa uwepo wa vyombo vya habari huru na vyenye ushawishi kama vile Sauti ya Amerika (VOA), Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Sauti ya Ujerumani (Deutshe Welle) kati ya mengine.

Hapa Kenya, serikali nyingi zimekuwa zikilaumiwa pakubwa kwa kuwatisha na kuwahangaisha raia wanaojitokeza kueleza hisia zao kuhusu masuala mbalimbali yanayoendelea nchini.

Mtindo huo ulianzishwa na serikali ya Mzee Jomo Kenyatta, marehemu Daniel Moi, Rais Mstaafu Mwai Kibaki na sasa Rais Uhuru Kenyatta.

Natoa urejeleo huu kufuatia madai ya mwanaharakati Boniface Mwangi, kwamba ametishiwa maisha na baadhi ya viongozi wenye ushawishi nchini kutokana na kauli ambazo amekuwa akitoa kuhusu vitendo vyao na mwelekeo wa nchi kwa jumla.

Bila shaka, hii si mara ya kwanza kwa mwanaharakati huyo kudai kutishiwa maisha yake na viongozi wenye ushawishi.

Wanaharakati wengine ambao washawahi kujipata katika hali hiyo ni Okiya Omtata, marehemu Wangari Mathai, Maina Kiai, aliyekuwa Jaji Mkuu Willy Mutunga, wakili Miguna Miguna kati ya wengine wengi.

Wakati wa utawala wa Bw Kibaki, nusura Bw Omtata apoteze maisha yake baada ya kukabiliwa vikali na polisi, akiitaka serikali kueleza jinsi Sh4.2 bilioni za Mpango wa Elimu Bila Malipo katika shule za msingi zilivyokuwa zimepotea.

Bw Omtata alipiga kambi katika makao makuu ya Wizara ya Eimu kwa siku saba, akiwaongoza wanaharakati wenzake kushinikiza serikali kueleza ukweli kuhusu sakata hiyo.

Kutokana na uanaharakati wake, ‘ahsante’ ya serikali ilikuwa kuwatuma polisi kumpiga kiasi cha kumvunja meno yake kadhaa.

Katika miaka ya tisini, marehemu Prof Mathai atakumbukwa kwa kuongoza harakati za kupinga uvamizi wa Msitu wa Karura jijini Nairobi na watu wenye ushawishi katika serikali ya Moi.

Kama Bw Omtata, utawala wa Moi ulituma polisi kumkabili Prof Mathai na kundi la wanaharakati alioukuwa akiwaongoza kupinga uvamizi huo.

Kama dhuluma za polisi hazikutosha, Bw Moi alimtusi kwa kumfananisha na mtu “aliyepagawa.”

Prof Mathai vile vile atakumbukwa kwa kuongoza harakati za kuushinikiza utawala wa Moi kuwaachilia wafungwa wa kisiasa kama vile aliyekuwa mbunge wa Subukia, Koigi wa Wamwere.

Bila shaka, visa hivi vinaashiria ukatili ambao serikali zimekuwa zikitumia dhidi ya yeyote anayeonekana kuzikosoa.

Tunapoelekea katika uchaguzi mkuu wa 2022, ni makosa makubwa wakati visa hivi vinapoanza kushuhudiwa. Wito wetu kwa serikali na asasi husika ni kuheshimu uhuru wa kila mtu kujieleza.

akamau@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

Real Sociedad watua kileleni mwa jedwali la Liga baada ya...

WANTO WARUI: Serikali isaidie kutafuta suluhu kwa visa vya...

F M