WANDERI KAMAU: Siasa zimeidunisha na kuteka taaluma ya uwakili

WANDERI KAMAU: Siasa zimeidunisha na kuteka taaluma ya uwakili

UWAKILI ni miongoni mwa taaluma zinazoenziwa na kuheshimika sana nchini.

Kando na udaktari, uwakili ni taaluma ambayo hutajwa sana na wanafunzi hao, kwani huwa ni kama ‘daraja’ kwa yeyote aliyesomea sheria kujiunga na Idara ya Mahakama nchini.

Mawakili pia ni miongoni mwa watu waliotoa mchango mkubwa nchini kwenye Vita vya Ukombozi wa Pili katika miaka ya 80’ na 90’ kukabiliana na utawala dhalimu wa marehemu Daniel Moi.

Mawakili mbalimbali waliungana na wahadhiri wa vyuo vikuu, wanahabari, wanasiasa na watetezi wa haki za binadamu kumshinikiza Moi kubadilisha sehemu 2(a) ya Katiba ili kuruhusu uwepo wa vyama vingi vya kisiasa.

Miongoni mwa wale waliojitokeza pakubwa kwenye harakati hizo ni mawakili watajika kama Gibson Kamau Kuria, Bi Martha Karua (kiongozi wa Narc-Kenya), Paul Muite, Seneta James Orengo, Gitobu Imanyara, Muturi Kigano, Gavana Kiraitu Murungi (Meru) kati ya wengine.

Wengi walifanikisha juhudi zao kupitia Chama cha Mawakili Kenya (LSK), kwani kilikuwa miongoni mwa mashirika yaliyojitokeza pakubwa kuungana na Wakenya waliokuwa wakipinga uongozi wa Kanu chini ya Bw Moi.

Harakati hizo ziliwainua sana mawakili nchini na kimataifa, hasa baada ya Moi hatimaye kukubali shinikizo alizopata kwa kurejesha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Walionekana kuwa watetezi wa haki, wasioogopa vitisho vyovyote kutoka kwa serikali au tawala zilizopo.

Hata hivyo, picha ya taaluma ya uwakili imekuwa ikiyumba katika siku za hivi karibuni, kutokana na malumbano na utepetevu mkubwa ambao umekuwa ukishuhudiwa katika LSK.

Viongozi wa chama hicho wamekubali kuwa mateka wa wanasiasa, hali ambayo imeshusha sana umaarufu wake na kuipaka tope taaluma hiyo kwa jumla.Mfano wa wazi ni aliyekuwa kiongozi mkuu wa chama hicho aliyeondolewa majuzi, Bw Nelson Havi.

Alipochukua uongozi wa chama mnamo 2019, Bw Havi aliahidi kuleta mwamko mpya chamani, kwa kurejesha sauti, hekima na ushawishi uliokuweko katika miaka ya ’90 kama mtetezi wa wanyonge.Hata hivyo, ahadi za Bw Havi ziligeuka kuwa sarakasi na mivutano kama iliyoshuhudiwa wakati wa ujenzi wa Mnara wa Babeli kwenye Biblia.

Badala ya kurejesha mwamko huo, Bw Havi alilaumiwa na baadhi ya wanachama kwa kuwa “kibaraka” wa baadhi ya wanasiasa.

Moja ya sababu waliyotoa ni hatua ya LSK kuwa miongoni mwa taasisi zilizojitokeza kupinga Mpango wa Kubadilisha Katiba (LSK).Kando na hayo, pengine kile kilichowashangaza wengi ni hatua ya Bw Havi kujitokeza wazi na kutangaza kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto na chama cha UDA.

Ametangaza atawania ubunge katika eneo la Westlands, Nairobi, kupitia UDA.Ingawa ni haki ya kidemokrasia ya Bw Havi kufuata mkondo wa kisiasa anaotaka, swali linaloibuka ni sababu yake kutojiondoa kwenye uongozi wa chama mapema wakati alipotangaza atajiunga na siasa.

Mbona ameondolewa kwa njia ya mivutano miongoni mwa wanachama? Alilenga kukitumia chama kujijenga kisiasa?Ni wakati uongozi mpya kuondoa tope lililopakwa chama hicho.

akamau@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

Azma ya Kalonzo itamfaidi mgombea mwingine, asema Kibwana

Wito wakulima washirikiane na kampuni za pembejeo kuzima...

T L