WANDERI KAMAU: Tutajinasua vipi kutoka kwa usahaulifu wetu?

WANDERI KAMAU: Tutajinasua vipi kutoka kwa usahaulifu wetu?

Na WANDERI KAMAU

NGIRI ni mnyama mwenye usahaulifu mkubwa sana. Ni kiumbe ambaye amekuwa akitumiwa kama mfano wa kuelezea athari za usahaulifu.

Usahaulifu ni udhaifu mbaya sana. Ni hali inayoweza kumrudisha mtu kwenye utumwa ama maovu aliyokuwa amejitoa kwayo.

Ni hali ambayo wazazi daima huwafunza wanao kujiepusha nayo, kwani huenda wakasahau misingi ya kimaadili waliyolelewa nayo.

Usahaulifu si hatari pekee kwa mtu binafsi. Ni hatari kwa mustakabali wa jamii, nchi ama falme. Ni hali inayoweza kuizamisha jamii kwenye mikasa, majanga ama maovu ambayo huenda ikawa vigumu kujitoa.

Natoa urejeleo huu kusawiri uhalisia ulio katika nchi yetu.

Tu nchi na jamii yenye usaulifu mkubwa. Tu watu wasiojua watokako na waelekeako. Tu taifa lililo kwenye hatari ya kupoteza thamani ya utaifa wake.

Sababu ya haya ni kuwa daima, huwa tunajipata kwenye matatizo na changamoto zilizotuandama zaidi ya miaka 40 iliyopita! Changamoto zinazotuandama ni mzunguko wa matatizo ya jana, leo, kesho, mtondo na mtondogoo.

Leo, mdahalo ulio katika kinywa cha karibu kila mtu ni siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2022. Kinaya ni kuwa, imebaki zaidi ya mwaka mmoja kabla ya uchaguzi huo kufanyika.

Taswira iliyo nchini ni kama kwamba tunaamkia uchaguzi mkuu kesho. Majibizano na cheche kali za maneno miongoni mwa wanasiasa tayari zimeanza kujenga taharuki za kisiasa katika baadhi ya maeneo nchini.

Watu wanaoonekana kuwa ‘wageni’ washaanza kupewa tahadhari kuhusu yale ambayo huenda yakawapata, ikiwa hawatarejea ‘makwao.’

Chini ya mazingira haya, kuna matatizo chungu nzima yanayoizonga nchi. Serikali za kaunti zinalalamika kutopewa fedha za kutosha kuendeleza majukumu yake. Wauguzi wanalalamika kutolipwa mishahara yao. Walimu wanatishia kugoma. Wanafunzi wanaendelea kuchoma shule.

Kama hayo hayatoshi, washirika wa Rais Uhuru Kenyatta, naibu wake William Ruto, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kati ya viongozi wengine wanaendelea kuzozana kuhusu ni nani “mwenye ushawishi mkubwa” kumliko mwenzake.

Kampeni za ripoti ya Mpango wa Maridhiano (BBI) zimeiteka nchi na kuwafumba macho wanasiasa kuhusu matatizo yanayowakumba wakulima, wafugaji na wafanyabiashara! Hakuna anayejali hata kidogo. Kila mwananchi anaubeba mzigo wake.

Chini ya mazingira hayo pia, janga la virusi vya corona linaendelea kuonyesha makali yake kama moto wa nyikani wakati wa kiangazi. Ingawa visa vya maambukizi vinaendelea kupungua, virusi hivi bado ni tishio kubwa kwa afya zetu.

Wiki chache zijazo, wanafunzi wa Darasa la Nane na Kidato cha Nne wanatarajiwa kuanza mitihani ya kitaifa. Hakuna anayeonekana kujali mazingira watakayofanyia mitihani yao yatakuwa vipi—yatakuwa tulivu ama yaliyojaa abrakadabra za ni mwanasiasa yupi maarufu na asiye maarufu?

Katika hali hii yote, tunaonekana kujitia hamnazo kuhusu athari za kutojali kwetu. Tushawahi kushuhudia matokeo ya hali hizi zote, upeo wake ukiwa ghasia za kikabila zilizoikumba nchi mwaka 2007/2008.

Hata hivyo, tu Jamhuri ya Usahaulifu. Taifa la Usahaulifu na Kutojali.

akamau@ke.nationmedia.com

You can share this post!

FAUSTINE NGILA: Tujizoeshe maisha ya dijitali

Wabunge wandani wa Ruto wapokonywa walinzi, bunduki