WANDERI KAMAU: Uamuzi kuhusu Sankara ulete mwanga mpya Afrika

WANDERI KAMAU: Uamuzi kuhusu Sankara ulete mwanga mpya Afrika

Na WANDERI KAMAU

SABABU nyingi ambazo zimekuwa zikichangia maovu kuendelea Afrika na nchi zenye chumi za kadri, ni kutochukuliwa hatua kwa viongozi waliohusika kwenye dhuluma za kijadi katika nchi zao.

Tangu mataifa hayo kujipa uhuru wao katika miaka ya sitini, mengi yamekumbwa na maovu mengi bila wahusika wakuu kukabiliwa kwa namna yoyote ile.

Maovu mengi huchangiwa na tamaa za mamlaka miongoni mwa viongozi wenye ushawishi.Matokeo ya tamaa hizo mara nyingi huwa ni mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, mapinduzi ya kijeshi au hata maafa.

Baadhi ya maovu ambayo hurejelewa kuwa miongoni mwa mikasa mikubwa iliyowahi kumkumba mwanadamu ni mauaji ya kimbari yaliyotokea Rwanda mnamo 1994, ambapo zaidi ya watu 800, 000 walipoteza maisha yao.Licha ya Afrika kuwekwa kwenye kapu la maeneo ambayo viongozi hufanya maovu bila kukabiliwa kwa namna yoyote kisheria, huenda dhana hiyo imeanza kuchukua mkondo mpya.

Hili linafuatia kufunguliwa mashtaka dhidi ya aliyekuwa rais wa Burkina Faso, Blaise Compaore, wiki hii kuhusiana na mauaji ya aliyekuwa kiongozi na mwanapinduzi maarufu wa kisiasa nchini humo, Thomas Sankara.

Mnamo Jumanne, mahakama ya kijeshi ilitangaza kuwa Compaore ana mashtaka ya kujibu kuhusu mauaji hayo yaliyofanyika 1987, baada ya kubainika kuna uwezekano alikuwa miongoni mwa wale waliohusika kwenye njama hizo.Compaore amekuwa uhamishoni nchini Ivory Coast tangu 2014, alipojiuzulu kama rais kutokana na maandamano makubwa ya raia dhidi ya uongozi wake.

Bila shaka, tangazo hilo limezua matumaini katika taifa hilo na barani Afrika kwa jumla, kwamba huenda mwanga ukaanza kupatikana kwa waathiriwa wote wa dhuluma za kijadi.K

abla ya mauaji yake ya kikatili, Sankara alikuwa miongoni mwa viongozi waliojizolea sifa kubwa barani na duniani kote, kutokana na juhudi zake katika kuwasaidia raia, hasa maskini. Anasifiwa kwa kuendeleza sera za kiuchumi zilizohakikisha usawa kati ya watu maskini na matajiri kati ya 1983 na 1987, alipoliongoza taifa hilo.

Kutokana na mwelekeo huo wenye matumaini, wito wetu ni kwa nchi zingine ulimwenguni kuiga Burkina Faso, kuhakikisha viongozi wote waliohusika kwa maovu ya awali wamekabiliwa kisheria bila huruma.

Hapa Kenya, wanasiasa wote waliohusika kwenye maovu kama vile uchochezi wa ghasia za kikabila lazima wakabiliwe.Hivyo ndivyo Afrika itapata mwanga na mwanzo mpya wa uwajibikaji miongoni mwa viongozi wake.

akamau@ke.nationmedia.com

You can share this post!

CHOCHEO: Jifunze kuomba msamaha ili furaha irejee kwenye...

Nia yetu ni kuisaidia Kenya kumudu madeni – IMF