WANDERI KAMAU: Wakati wa Kenya kuonyesha imeiva kidemokrasia ni sasa

WANDERI KAMAU: Wakati wa Kenya kuonyesha imeiva kidemokrasia ni sasa

NA WANDERI KAMAU

MACHO yote kote duniani yataelekezwa Kenya kutathmini namna itaendesha uchaguzi wake mkuu.

Huu ni uchaguzi wa kipekee nchini, kwa kuwa unahusu mabadiliko ya kiutawala kutoka serikali moja hadi nyingine.Ni uchaguzi unaofanana ule wa 2002 na 2013.

Mnamo 2002, ilikuwa mara ya kwanza kwa Wakenya kumchagua kiongozi wa upinzani kama rais wao.

Wakenya walimchagua hayati Mwai Kibaki kama “ghadhabu” dhidi ya uongozi wa marehemu Daniel Moi na utawala wa chama cha Kanu kwa jumla.

Hivyo, mnamo 2002, ilikuwa kama maasi dhidi ya Kanu kutokana na mateso mengi ambayo mamilioni ya raia walikuwa wakipitia.Sawa na sasa, hali ya kiuchumi wakati huo ilikuwa mbaya.

Ilikuwa vigumu kwa Wakenya wengi kupata bidhaa za matumizi ya msingi kutokana na sera mbovu za kiuchumi na kisiasa zilizoendeshwa na utawala wa Kanu.

Hata hivyo, viongozi wa Kanu walijitia hamnazo, kwa kutojali hali ilivyokuwa nchini.Kile walichotilia mkazo ni “kuendeleza uaminifu wao” kwa utawala wa Moi.

Kama 2002, Wakenya walipiga kura mnamo 2013 kama maasi dhidi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), kutokana na mashtaka ya uhalifu wa kibinadamu yaliyokuwa yakiwakabili Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais William Ruto na Wakenya wengine wanne katika mahakama hiyo.

Hili lilitokana na ghasia zilizotokea nchini kufuatia uchaguzi tata wa urais 2007.

Kufuatia maamuzi ya 2013, funzo kuu ambalo Kenya imepata ni kuwa, kiupana, Rais Kenyatta na Dkt Ruto hawakuunganishwa na mpango waliokuwa nao kuibadilisha nchi, bali na mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili katika ICC.

Hili limedhihirishwa na tofauti kali ambazo zimeibuka kati ya viongozi hao wawili.

Hadi sasa, uchaguzi huu unaonekana kuandamwa na tofauti baina ya viongozi hao, kuliko ushindani kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto.

Ni wazi kuwa, muhula wa pili wa utawala wa Rais Kenyatta utakumbukwa kwa ushindani na mivutano ya kisiasa baina yake, Dkt Ruto na Bw Odinga, wala si mipango iliyoendeshwa na serikali kuboresha maisha ya Wakenya.

Kwenye uchaguzi wa kesho Jumanne, Wakenya wanafaa kuhakikisha, wanapiga kura kulingana na utendakazi wa kiongozi husika, wala si wimbi fulani la kisiasa.

Waepuke misukumo yoyote ya kisiasa, ili kuhakikisha hawajutii maamuzi watakayofanya baadaye. Wasizingatie mawimbi yanayoletwa na viongozi wala vyama vya kisiasa.

akamau@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

Jinsi vijana, wanamuziki walivyopiga kampeni za Azimio eneo...

TALANTA: Watoto wa familia moja waliobobea kwa nyimbo

T L