WANDERI KAMAU: Wakenya wachukulie kwa uzito mchakato wa kuchagua viongozi

WANDERI KAMAU: Wakenya wachukulie kwa uzito mchakato wa kuchagua viongozi

NA WANDERI KAMAU

IDADI ndogo ya Wakenya waliojitokeza Jumanne kushiriki katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, inaashiria kuwa kiwango kikubwa cha watu wamepoteza imani na uongozi pamoja na upigaji kura nchini.

Wengine walinukuliwa wakisema kuwa, walishiriki kwenye zoezi hilo ili “kuwaadhibu” baadhi ya viongozi waliohisi hawakuwasaidia kwa vyovyote vile kwa muda waliohudumu.

Wakati kunakuwa na wananchi wanaotoa kauli kama hizo, hiyo ni dalili ya wazi kuwa mchakato wa upigaji kura unaendelea kupoteza maana yake nchini.

Kimsingi, upigaji kura unapaswa kuwa nafasi nzuri kwa wananchi kufanya maamuzi muhimu yatakayohakikisha kuwa wanaishi maisha mazuri katika mazingira bora.

Ni kwenye mazingira hayo ambapo wao hupata nafasi kuboresha na kujiendeleza kimaisha katika fani zote za maisha.

Cha kusikitisha ni kuwa, wale wanaoonekana kupoteza maana ya kupiga kura ni vijana.

Hilo si tu kutokana na idadi yao ndogo iliyojitokeza kupiga kura, bali hata idadi iliyojitokeza kusajiliwa kama wapigakura mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022.

Upigaji kura huwa jambo linalopewa uzito mkubwa na mataifa yaliyostawi kiviwanda kama Amerika. Kila baada ya miaka minne, uchaguzi wa urais nchini humo huwa jambo kubwa ambalo huzua msisimko wa aina yake, kutokana na uzito wake kwa raia wote, bila kuzingatia ikiwa wao ni vijana au wazee.

Vivyo hivyo, Wakenya wanafaa kutathmini tena msimamo wao kuhusu upigaji kura, kwani ndiyo njia pekee itakayoboresha mustakabali wa taifa hili.

Kwa sasa, hali hii ambapo vijana wanajitenga na mchakato mzima wa kuchagua viongozi inaleta wasiwasi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ijayo isuluhishe upesi mzozo na FIFA,...

Magoha asogeza tarehe ya wanafunzi kurudi shuleni

T L