WANDERI KAMAU: Wanawake ni thawabu kuu tunayofaa kujivunia

WANDERI KAMAU: Wanawake ni thawabu kuu tunayofaa kujivunia

Na WANDERI KAMAU

NINAPOWATAZAMA watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa wakiwadhulumu wanawake, huwa ninasikitika sana.

Pengine huwa wanasahau majukumu ambayo wanawake hutekeleza maishani mwetu.Wanawake ni kama ‘miungu’ wetu hapa duniani. Wao ndio ‘daraja’ la uhai kati ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu.

Je, tungekuwa wapi ikiwa wangeamua kukatisha uhai wetu walipokuwa wametubeba wakati wa ujauzito wao?Jukumu ambalo wanawake hutekeleza katika kuleta uhai wa mwanadamu ni la kipekee.

Ni jukumu ambalo halipaswi kupuuzwa hata kidogo.Utotoni mwangu, nilimtazama mama yangu akiamka mapema kila siku kututayarisha tulipokuwa tukienda shuleni.

Baada ya hapo, angeanza kazi za nyumbani kama kutayarisha staftahi, kukamua ng’ombe, kuosha vyombo, kuchota maji, kuwapikia jamaa walioachwa, kwenda kulima kati ya kazi nyingine. Majukumu yake hayakuishia hapo.Tuliporudi nyumbani, mama hangepumzika.

Ingawa wakati mwingine tulisaidiana naye, bado alitekeleza majukumu mengi ili kutupa muda wa kutosha kusoma na kufanya mazoezi tuliyokuwa tukipewa shuleni.

Katika hali hiyo, ni wazi kuwa wanawake ni viumbe spesheli ambao kila mwanadamu anapaswa kuwaheshimu katika kila hatua ya maisha yake.Sidhani ni makosa kuwataja wanawake kuwa ‘mabalozi’ na ‘wawakilishi’ wa Mungu hapa duniani.

Licha ya majukumu hayo, inasikitisha kuwa jamii mbalimbali duniani bado zinaendelea kuwabagua, kuwatenga na kuwadhulumu wanawake na kuwaona kama viumbe duni wasiofaa kupewa nafasi yoyote katika maendeleo ya jamii husika.

Dhana hii ya kumdunisha mwanadamui ilishuhudiwa katika karne za 17, 18 na 19, wakati Wazungu, Waarabu na Wareno walivamia himaya mbalimbali barani Afrika kuwatafuta watumwa wa kufanya kazi katika nchi zao.

Cha kusikitisha ni kuwa, ubaguzi wa wanawake ulianza nyakati hizo.Baada ya watu hao kuvamia kijiji ama vijiji husika, walikuwa wakiwabaka wanawake na kuwageuza kuwa watumwa wa ngono, kulingana na vitabu na simulizi nyingi za historia zilizopo.

Baadaye, wangewateka wanaume na vijana barobaro na kuwasafirisha katika nchi zao kufanya kazi kwenye mashamba na viwanda.

Wanawake ndio walioachiwa majukumu ya kuwalea wanao kama wajane. Wengi walijikaza na kuwalea watoto wao hadi utu uzima katika mazingira magumu sana.

Ingawa makala haya hayalengi kuwadunisha wanaume na michango wanayotoa katika jamii, lengo lake ni kuihamasisha jamii kuwa wanawake ni viumbe wanaostahili kukwezwa ili kufikia upeo wa malengo na matamanio yao.

Vivyo hivyo, ingawa si wote waadilifu na wanaostahili sifa hizi, ukweli ni kuwa asilimia kubwa ya wanawake wetu ni kama thawabu katika maisha yetu.

Tusingekuwepo ikiwa si michango na malezi bora waliyotupa.Binafsi, singefikia nilipo isingekuwa ni michango muhimu ya wanawake mbalimbali kama mwalimu wangu wa chekechea.

Huyo ndiye aliyeweka msingi wa kiusomi katika maisha yangu.Kwa michango hiyo, ni makosa makubwa kwa jamii kuendeleza ubaguzi dhidi ya wanawake kwa misingi ya kisiasa, kiuchumi, kidini ama kitamaduni.

Wanawake ni zawadi maalum ambazo tunapaswa kuzitunza katika kila hali.Kama shukrani kwao, jamii zinapaswa kubuni sheria kali zinazowakabili wale wanaowadhulumu wanawake kwa vyovyote vile.

You can share this post!

Corona: Kifo cha polisi chaanika mahangaiko

KINYUA BIN KING’ORI: Raia wawe macho wasichague...