Makala

WANDERI: Kanisa lisiwe mateka wa wanasiasa nchini

September 10th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

UTAKATIFU wa maabadi ni nguzo kuu inayozingatiwa na dini zote hapa duniani.

Licha ya tofauti za kimafundisho zilizopo baina yao, uwiano mkuu uliopo kwenye kanuni zake ni kuwa mahali pa kuabudia ni patakatifu na lazima paheshimiwe kwa namna yoyote ile.

Uwiano mwingine wa kimafundisho ni kuwa lazima washiriki wawaheshimu viongozi wa kidini, kwani wengi huchukuliwa kuwa daraja kuu kati ya Mungu na mwanadamu.

Hivyo, haijalishi ikiwa kiongozi wa kidini ni Mkristo, Mwislamu, Mhindi ama Mbuddha; fundisho kuu katika dini zote ni kuwa lazima waheshimiwe kutokana na majukumu muhimu wanayotekeleza katika jamii.

Hata hivyo, hali inaonekana kubadilika nchini, hasa midahalo ya kisiasa inapozidi kuongezeka kuhusu urithi wa Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2022.

Wanasiasa wameyateka makanisa na kuyageuza majukwaa ya kuendeleza mashindano ya kisiasa kati ya mirengo tofauti wanayoegemea.

Kwa mfano, mnamo Jumapili, kizaazaa kikali kilizuka katika Kanisa la Katoliki la Gitui, eneobunge la Kiharu, Kaunti ya Murang’a, baada ya mbunge wa eneo hilo Bw Ndindi Nyoro kukabiliana vikali na Mbunge Maalum Maina Kamanda.

Bw Nyoro, ambaye anaegemea upande wa kundi la Tanga Tanga ambalo linamuunga mkono Naibu Rais Wiliam Ruto, alisema kuwa Bw Kamanda na wabunge wa kundi la Kieleweke waliingia katika eneobunge hilo bila ‘ruhusa yake.’

Ni mzozo uliowalazimu polisi kuingilia kati na kuwatuliza wafuasi wa mirengo hiyo miwili shindani kisiasa.

Katika kizaazaa hicho chote, kilichosikitisha zaidi ni kuwa kilifanyika kanisani, huku viongozi wa kanisa husika wakionekana kushindwa kabisa kuwazuia wanasiasa hao dhidi ya kurushiana cheche za matusi.

Kinachoibuka ni kuwa kanisa nchini limeshindwa kabisa kusimama kidete na kueleza msimamo wake kuhusu masuala mbalimbali yanayoihusu nchi.

Badala yake, viongozi wake wengi wamejipata kama mateka wa kisiasa wakirushwa kila upande kama vinyago bila kuwauliza maswali wanasiasa hao.

Pesa zimegeuka nta ambayo imewaziba vinywa na akili zao kiasi kwamba hawawezi kueleza ama kutoa misimamo huru, ikizingatiwa wanawaongoza mamilioni ya Wakenya wanaoshiriki katika makanisa yao.

Viongozi wa makanisa lazima wawaige wenzao kama marehemu maaskofu Alexander Kipsang Muge, Manasses Kuria na Henry Okullu. Katika miaka ya themanini na tisini, wakati walipohudumu, kanisa lilikuwa likitoa msimamo huru kuhusu hali ya kisiasa ilivyokuwa nchini bila kuwaogopa viongozi.

Ni wakati viongozi waliopo kama maaskofu wastaafu Timothy Njoya na Ndingi Mwana a’Nzeki kusimama na kulizindua upya kanisa kuhusu umuhimu wa kuonyesha misimamo huru.

Ni lazima wasimame ili kuwakumbusha viongozi wa sasa kwamba wakati msambao wa kanisa ulianza katika karne za 17 na 18, wanaharakati waliotetea na kusimamia ukweli kama Martin Luther King, Ulrich Zwingli, John Huss kati ya wengine waliuawa kwa misimamo yao huru.

La sivyo, kuna hatari ya msingi na usemi wa kanisa kuisha nchini, ikiwa hali ya sasa haitadhibitiwa.

[email protected]