Makala

WANDERI: Mauaji ya zamani yachunguzwe kuanika waliohusika

December 20th, 2018 2 min read

Na WANDERI KAMAU

HATUA ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji kuirai mahakama kuchunguza kilichosababisha kifo cha aliyekuwa Gavana wa Nyeri, Dkt Wahome Gakuru (pichani) inapaswa kufungua ukurasa mpya kuhusu mauaji ya awali nchini.

Katika ombi lake, Bw Haji anasema anaamini kwamba ukweli kuhusu kifo cha Dkt Gakuru utapatikana kikamilifu ikiwa itashiriki moja kwa moja katika mchakato huo.

Ni ombi ambalo limezua hisia mseto, huku baadhi ya watu wakiitaka DCI kuanzisha uchunguzi wa mauaji tata ya awali ambayo yamesalia fumbo hadi sasa.

Miongoni mwa wale ambao wametangaza hilo ni aliyekuwa kamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Dkt Roselyn Akombe, anayesema kwamba yuko tayari kutoa ushahidi kuhusu mauaji ya aliyekuwa msimamizi wa mitambo (ICT) katika tume hiyo, Chris Msando.

Bila shaka, kilicho wazi ni kwamba michakato ya uchunguzi wa mauaji tata nchini huisha katika njia zisizoeleweka, huku watuhumiwa wakuu wakiendelea na maisha yao kama kawaida.

Tangu tulipojinyakulia uhuru, tumeshuhudia mauaji ya watu maarufu ila hadi sasa, ni watu wachache ambao wamehukumiwa kuhusiana nayo.

Miongoni mwa waliouawa katika njia tatanishi ni aliyekuwa mwanaharakati wa kisiasa Pio Gama Pinto, wanasiasa Tom Mboya, Josiah Mwangi Kariuki (JM), Dkt Chrispine Mbai, mwanasiasa Robert Ouko kati ya wengine.

Katika baadhi ya visa hivi, wanasiasa wenye ushawishi ndio wametajwa kuwa wahusika wa moja kwa moja.

Wanadaiwa kupanga mauaji dhidi ya wenzao kwa kuwachukulia kama ‘tishio’ kwa mistakabali yao ya kisiasa.

Kwa mfano, mwanasiasa JM Kariuki anadaiwa “kuondolewa” baada ya kuwakasirisha baadhi ya viongozi wakuu katika serikali ya hayati Mzee Jomo Kenyatta kwa kusema kuwa Kenya ilikuwa ya “mamilionea kumi na omba omba milioni kumi.”

Naye Dkt Ouko, ambaye alihudumu kama Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje alidaiwa kuuawa kwa madai ya “kufichua siri za serikali” ya Rais Mstaafu Daniel Moi kwa nchi za Magharibi mnamo 1990.

Kwa hayo, ombi langu ni kwamba mauaji hayo yanapaswa kuchunguzwa upya ili kubaini wale waliohusika kwenye mauaji hayo. Hatuwezi kuendelea kuishi katika jamii iliyowaficha waovu wanaofahamika wazi.

Ni kupitia hilo ambapo haki itapatikana kwa familia, jamaa na marafiki wa viongozi hao.

[email protected]