Makala

WANDERI: Muda umefika Wakenya kuungana ili kujikomboa

September 5th, 2018 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MNAMO Agosti 10, 1792 mfumo wa kifalme ulifikia mwisho nchini Ufaransa, baada ya maandamano makubwa ya wakulima dhidi ya viwango vya juu vya kodi walivyokuwa wakitozwa.

Wakulima waliandamana na kupiga kambi katika Ikulu ya Mfalme Louis 16, wakilalamikia kiwango kikubwa cha fedha ambacho ufalme ulikuwa ukitumia ili kuendesha maisha ya kifahari, huku wao wenyewe wakiishi katika maisha ya kichochole.

Ujumuisho wa raia wa Ufaransa wakati huo ni kuwa zaidi ya asilimia 80 walitegemea kilimo, hivyo walihisi makali ya kiwango hicho cha kodi.

Kwa ghadhabu ya kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama mkate, maandamano hayo yalipelekea kuisha kwa mfumo wa kifalme na kuanza kwa utaratibu mpya wa kiutawala uliowashirikisha raia wote.

Cha msingi ni kwamba, watu hawakuungana tu; ila kando na matatizo ya kiuchumi yaliyowakabili, waliwategemea sana wasomi na wanafalsafa ambao waliwapa mwanga kuhusu udhalimu wa mfumo wa kifalme.

Baadhi ya wanafalsafa hao wenye mawazo ya kimapinduzi ni kama Voltaire, Jean-Jacques Rousseau, Denis Diderot kati ya watu wengine wengi.

Mapinduzi hayo ya kiraia yalichangia pakubwa katika ujio wa viongozi kama Napoleon Bonaparte, aliyeibukia kuwa maarufu sana katika historia ya kimapinduzi ya Ufaransa.

Kwa sasa, Kenya iko katika njia panda ya kisiasa, hasa inapoelekea mwaka 2022.

Wengi wanalalamikia ugumu wa maisha, hasa baada ya Serikali kuongeza asilimia 16 ya kodi kwa mafuta na kuathiri bidhaa zote zinazohusiana nayo.

Hili bila shaka limewaacha Wakenya katika njia panda ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kuhusu wanakoelekea kutokana na ugumu wa kimaisha.

Kwanza, kilicho dhahiri ni kwamba, kama ilivyokuwa Ufaransa, kuna uwezekano mkubwa kwamba safari ya mapinduzi ya kiraia nchini itaanza karibuni.

Huu ndio wakati mwafaka zaidi ambapo Wakenya wanapaswa kuungana dhidi ya mfumo wa kitabaka ambao umetumiwa na famillia za kisiasa kuwakandamiza kwa msingi wa kuwafarakanisha.

Kwa mfano, wafuasi wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga walijawa matumaini kwamba mwafaka wa kisiasa kati yao ungezaa matunda.

Kuna wale walioshangilia kwamba hatimaye ‘matunda’ waliyokuwa wakitafuta wameyapata. Wengine walifurahi kwamba “usumbufu” wa adui yao umeisha.

Ni maswali mengi ila hali ilivyo, imefikia wakati Wakenya kuzinduka na kuanza mapinduzi ya kiraia.

Kama anavyorejelea msomi Frantz Fannon (kwenye kitabu Wretched of the Earth-Watengwa wa Dunia) tabaka la kundi la chini litabaki mateka wa mabwanyenye waendesha uchumi ikiwa halitajitokeza na kupigania haki zao.

Katika maasi ya Kiarabu yaliyoanza mnamo 2011, uchunguzi wa kina umebainisha kwamba ingawa kulikuwa na shinikizo za kisiasa, mojawapo ya sababu kuu ilikuwa ni shinikizo za kupanda kwa bei za msingi kama mkate jinsi Kenya ilivyo kwa sasa.

Imefikia wakati Wakenya kuungana bila kujali tofauti zao za kikabila, kisiasa, kidini, kitamaduni kusema “Yametosha”!

Si Uhuru, Raila ama Ruto atawaokoa. Njia ni moja; kuungana na kuanza safari ya ukombozi.

[email protected]