MakalaSiasa

WANDERI: Nani aliroga wanasiasa wa Kenya? Kazi yao ni domodomo tu!

July 24th, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MALUMBANO, mizozo na ushindani mkubwa miongoni mwa wanasiasa unaweza kumfanya mtu kudhani tunaamkia uchaguzi mkuu kesho huku wanasiasa wakiandaa mikutano ya siasa bila kujali hatari ya virusi vya corona inayoikumba nchi na dunia nzima.

Pindi baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuondoa marufuku ya kutosafiri mapema mwezi huu, baadhi ya watu walifurahia hatua hiyo kama “Siku ya Ukombozi.”

Matokeo ya vitendo yake yamekuwa ni ongezeko la maambukizi ya virusi. Hata hivyo, hofu kuu ni kiwango cha kutojali miongoni mwa wananchi wanaoshinikizwa kuhudhuria mikutano na wanasiasa hao.

Kwa mfano, katika eneo la Magharibi, kuna makundi mawili yanayozozania “uongozi” wa jamii ya Abaluhya, moja likiwashirikisha Gavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (COTU) Francis Atwoli.

Kundi pinzani linawajumuisha kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na Seneta Moses Wetang’ula (Bungoma), ambaye pia ndiye kiongozi wa Ford-Kenya.

Katika eneo la Bonde la Ufa, kumezuka makundi mawili pia – linalomuunga mkono Naibu Rais William Ruto kuwania urais 2022 na lile ambalo limetangaza kumuunga Seneta Gideon Moi (Baringo) kuwania nafasi hiyo.Katika eneo la Mlima Kenya, hali ni sawa. 

Kumeibuka karibu makundi manne ya kisiasa, ambapo yote yanadai kuweka mikakati kuhusu “urithi” wa Rais Kenyatta.

Makundi hayo ni ‘Tangatanga’; linalowajumuisha wabunge ambao wamekuwa wakimpigia debe Dkt Ruto, ‘Kieleweke’; linaloongozwa na mbunge Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini) na linalodai “kumlinda na kumtetea” Rais Kenyatta, kundi pinzani linaloongozwa na mbunge Kanini Keega (Kieni) na la mwisho, ambalo limetangaza kumuunga mkono mwanasiasa Peter Kenneth kumrithi Rais Kenyatta kama kiongozi wa eneo hilo.

Bila shaka, kwa taswira kama hiyo, nchi imegeuka kuwa kama uwanja wa vita.

Imekuwa kama Mnara wa Babeli, ambapo Mungu alikasirishwa na wajenzi wake na kuwavuruga kwa kuweka tofauti za lugha baina yao.

Ijapokuwa mwanadamu ni kiumbe apendaye siasa kimaumbile, ni mapema sana kuanza kuendeleza siasa karibu miaka miwili kabla ya uchaguzi.

Matokeo ya ushindani huu utakuwa ni ujenzi wa taharuki na chuki za kisiasa na kikabila zisizofaa, ambapo mwananchi ndiye atakuwa mwathiriwa mkuu.

Inapasa viongozi wa Kenya wajifunze na nchi zilizostawi kiuchumi na kisiasa kama Uingereza, ambako kuna wakati maalum wa kufanya siasa.

[email protected]