MakalaSiasa

WANDERI: Rais binafsi ajipe jukumu la kuzima ufisadi

December 18th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

AGIZO la Rais Uhuru Kenyatta kuwa maafisa wa serikali hawapaswi kujiingiza katika biashara ama utoaji huduma zinazohusiana na taaluma zao kwa umma linapaswa kukumbatiwa na kila mmoja.

Ni dhahiri kuwa kwa muda mrefu, Wakenya wamekuwa wakilalamikia kudorora kwa huduma zinazotolewa katika taasisi za umma kutokana na uzembe wa maafisa hao.

Kama hilo halitoshi, wengine hata wamekuwa wakifanya biashara na asasi mbalimbali za serikali, hasa katika kiwango cha kaunti.

Kando na hayo, baadhi hutumia ushawishi wao kuhakikisha kuwa kampuni zao ama washirika wao wa karibu ndizo zinazopewa kandarasi na serikali.

Kwa mtindo huo, imekuwa vigumu kukabili mtaasisiko wa ufisadi katika taasisi kuu za serikali.

Kwa urejeleo wa kina, agizo la Rais Kenyatta si la kwanza, kwani lilitolewa kwa mara ya kwanza na Tume ya Ndegwa mnamo 1970. Tume hiyo ilibuniwa na Mzee Jomo Kenyatta kutathmini ulainishaji wa utendakazi miongoni watumishi wa serikali.

Kwenye ripoti yake mnamo 1971 , tume ilipendekeza kupigwa marufuku kwa wafanyakazi wa serikali kufanya biashara yoyote na asasi za serikali.

Lengo la pendekezo hilo lilikuwa kuwazuia wafanyakazi hao kujitajirisha kupitia biashara ama kandarasi zinazotolewa na serikali.

Hata hivyo, hali imekuwa kinyume kwani licha ya pendekezo hilo, ni kawaida kwa maafisa wa serikali kushiriki biashara za kila aina na Serikali Kuu.

Kinaya ni kwamba, wale ambao hushindwa kufanya hivyo huonekana kama “wajinga ambao hawajaerevuka.”

Mbinu hii ndiyo imekuwa ikitumika na wafanyakazi wa serikali kuifyonza mamilioni ya pesa bila kujali hata kidogo.

Kwenye makumi ya sakata za ufisadi ambazo zimefichuliwa na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC), Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), imefichuka kuwa maafisa wa ngazi za juu kama magavana hutumia mawakala wao kuzipora kaunti.

Kwenye njama hizo, huwa wanasajilisha kampuni zao binafsi kwa kuwatumia mawakala hao kama “wamiliki” ambapo baadaye huwa wanagawana pesa wanazopata kandarasi kwa njia za mkato.

Njama hiyo ndiyo ilidhihirika kwenye sakata kama ile ya Shirika la Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS) na kaunti mbalimbali ambapo maafisa wake wakuu wanakabiliwa na tuhuma za ufisadi.

Ilivyo sasa, lazima serikali ichukue hatua badala ya kuendelea kusema na kusema. Hali lazima ibadilike iwe kusema na kutenda. Ufisadi nchini umegeuka kuwa saratani ambayo huenda ikawa vigumu kuitibu.

Kando na hatua zinazoendeshwa na asasi husika, lazima Rais Kenyatta mwenyewe ahakikishe kuwa anashiriki binafsi kwenye vita hivyo bila mwingilio ama mapendeleo yoyote ya kisiasa.

Nchi ambapo marais wamechukua jukumu hilo mikononi mwao zimepata mafanikio makubwa.

Baadhi ya viongozi hao ni Rais John Magufuli wa Tanzania, rais wa kwanza wa Botswana Seretse Khama, Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino kati ya wengine.

Hiyo ndiyo njia pekee Kenya itafaulu.

[email protected]