Makala

WANDERI: Tusife moyo, saratani bado yaweza kuzimwa

July 28th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

SARATANI ni muuaji. Ni Malaika Izraili. Ni Malaika wa Kifo ambaye ukatili wake lazima ukomeshwe.

Ukatili wake umeitikisa nchi kwa kuwanyakuwa tu watu ambao ni nguzo kuu ya jamii. Ni kama mwewe mwenye njaa, ambaye hunyakua na kuwaua vifaranga wadogo ambao bado hawajakomaa.

Uhayawani wake umesababisha majonzi kwa jamaa, rafiki na familia za watu aliowanyakuwa hata bila kuwapa ishara.

Kenya inaomboleza mashujaa wawili walionyakuliwa na kuuliwa na zimwi hili hatari.

Katika mwezi huu wa Julai pekee, wametuacha Bob Collymore na mbunge wa Kibra, Bw Kenneth Okoth.

Wawili hao wamenyakuliwa na Izraili Saratani, hata baada ya kupokea matibabu.

Bw Collymore alifariki mapema mwezi huu baada ya kuugua saratani ya damu, huku Bw Okoth akifariki mnamo Ijumaa, baada ya kuugua saratani ya maini.

Wote walikuwa watu muhimu, waliotegemewa na maelfu katika jamii. Bw Collymore alikuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya Safaricom, ambayo ni mojawapo ya zile zinazopata faida kubwa zaidi katika eneo la Afrika Mashariki.

Kampuni hiyo ina zaidi ya wateja 30 milioni, kumaanisha kuwa Collymore alikuwa “baba” ya Wakenya 30 milioni ambao wanatumia huduma za kampuni hiyo kwa njia moja ama nyingine.

Na kama mbunge wa Kibra, Ken alikuwa “baba” ya zaidi ya wakazi 178,000 wa eneo hilo—kumaanisha kwamba Izraili Saratani ametupokonya watu wawili waliotegemewa na mamilioni ya Wakenya.

Kando na vifo vya wawili hao, nchini kote mmefichika maelfu ya simulizi za kuogofya, kuhusu vile familia nyingi zimewapoteza wapendwa wao kutokana na ugonjwa huu hatari.

Baadhi ya familia zimelazimika kuwatazama jamaa zao wakifia vitandani mwao kwa kukosa fedha za kugharamia matibabu yao ya hospitali. Wengine wamekwama katika nchi za kigeni kama India, baada ya kushindwa kulipa madeni ya matibabu ya jamaa zao. Wengine pia wameamua kuwatelekeza jamaa zao wanaougua ugonjwa huo, kwa kuuona kama laana kwao.

Simulizi hizi zote zinaonyesha nchi ambayo msingi wake umetikisika. Zinaonyesha jamii ambayo imekata tamaa ya maisha; ilmradi Izraili huyu akupatapo, matumaini ya maisha hukatika papo hapo.

Licha ya hali hizi zote, lazima asasi zetu zibaini jinsi makali ya ugonjwa huu yatakabiliwa. Maombolezo ya kila mara hayatatusaidia, ila ni mikakati thabiti itakayohakikisha kuwa kila Mkenya anamudu gharama ya matibabu yake bila kujali kiasi cha mapato yake.

Hatua ya kwanza ni kuutangaza ugonjwa huu kama janga la kitaifa. Kwa hili, serikali inapaswa kubuni hazina maalum ya kitaifa ambayo itakuwa kama bima ya kugharamia matibabu ya Wakenya wote wanaopatikana kuugua ugonjwa huu. Ndivyo yamefanya mataifa kama Singapore na Japan.

Pili, ni lazima serikali ishirikiane na wadau kubuni vituo vya utafiti kuhusu viini vya ugonjwa huo. Vile vile, lazima ibuni mkakati wa kitaifa kuwahamasisha Wakenya kuhusu umuhimu wa kula vyakula asilia.

[email protected]