Makala

WANDERI: Ukakamavu wa Omido ni fahari kuu kwa Maathai

July 21st, 2020 2 min read

Na WANDERI KAMAU

FLORENCE Nightingale anakumbukwa duniani kote kama mwanzilishi taaluma ya uuguzi karne 19.

Alizaliwa Uingereza 1810 kwenye familia tajiri jijini London, lakini akakaidi maagizo ya wazazi wake kutosomea uuguzi.

Kwenye nafsi yake, Florence aliamini uuguzi ni taaluma inayochangia pakubwa katika kusaidia jamii.

Licha ya taaluma hiyo kupuuzwa na makundi ya watu matajiri nchini humo, mchango wa Florence ulidhihirika kwenye vita vilivyotokea kati ya muungano wa Uingereza, Ufaransa, falme za Ottoman na Saldinia dhidi ya Urusi kati ya 1853 na 1856.

Kwenye vita hivyo, wauguzi wanawake ndio walipelekwa katika maeneo ya vita na Florence kuwatibu maelfu ya wanajeshi waliojeruhiwa.

Hilo halikuwa likifanyika awali.Kutokana na mchango huo, alipewa tuzo maalumu na Malkia Victoria wa Uingereza ili kumshukuru kwa mchango mkubwa aliotoa kwa wanajeshi.

Florence ni mfano wa jinsi wanawake katika jamii wanatekeleza majukumu muhimu bila wengi kuwachukulia kwa uzito.

Wengi wametumia ujuzi wao kuziokoa jamii dhidi ya athari za majanga makubwa, lakini huonekana tu kama viumbe dhaifu wasio na umuhimu wowote.

Hivyo, makala haya yanalenga kutambua michango ya wanawake binafsi nchini, hasa wale wamejituma bila kuogopa vikwazo na pingamizi wanazowekewa na wale wasiofurahishwa na juhudi zao.

Hasa, yanalenga kumpa utambuzi maalum Bi Phyllis Omido, ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kuwatetea wakazi wa mtaa duni wa Owino Uhuru, eneobunge la Jomvu, Kaunti ya Mombasa dhidi ya athari za sumu ya madini ya risasi.

Athari zimekuwa zikichangiwa na viwanda kadhaa vya kutengeneza madini hayo katika eneo hilo.

Chini ya uongozi wa Bi Omido, wakazi waliishtaki rasmi serikali mnamo 2016 kwa kutochukua hatua za kutosha kuwalinda dhidi ya athari hizo, licha yao kuwasilisha malalamishi kwa idara nyingi zinazohusika na masuala ya mazingira.

Upeo wa malalamishi yao ulikuwa uamuzi wa Mahakama ya Mazingira ya Mombasa, Alhamisi iliyopita, kuwa serikali iwalipe wakazi Sh1.3 bilioni kama fidia katika miezi minne ijayo.

Ingawa ni fumbo ikiwa serikali itatii agizo hilo, uamuzi huo unaonyesha wanawake wanaweza kuwa watetezi halisi wa jamii.

Ushujaa ambao Bi Omido ameonyesha kwenye utetezi wa wakazi ni wa kupigiwa mfano, kuwa juhudi za wananchi binafsi zinaweza kuzikomboa jamii dhidi ya madhila zinayopitia.

Ikiwa angekuwa hai leo, naamini Prof Wangari Mathai angekuwa miongoni mwa watu ambao wangemfaharikia sana Bi Omido, kwa kuendeleza harakati za kutetea mazingira.Katika wakati huu ambapo jamii inaendelea kushuhudia ongezeko la maovu na dhuluma dhidi ya wanawake kama kupachikwa mimba kwa wasichana wadogo, ni lazima sauti zao zisikike.

Bi Omido amejitokeza kama mwanga mkuu kwao, kwamba kinachohitajika kwenye juhudi zao ni ushujaa na kujitolea.Hawapaswi kufunikwa na taasubi za kiume na dhana za kikale eti wao ni viumbe dhaifu.

[email protected]