Makala

WANDERI: Umefika wakati wa kuwaadhibu wauaji hawa

February 7th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MAUAJI ya kinyama ya mwanadada Mildred Odira wiki iliyopita, yameibua tena hali ya kukithiri kwa mauaji ya kikatili nchini, huku washiriki wakuu wakionekana kutofikiwa na mkono wa sheria.

Bi Odira, ambaye alikuwa mtaalamu wa simu katika kampuni ya habari ya Nation Media Group (NMG) alitekwa nyara katika hali tatanishi, ambapo mwili wake ulipatikana badaye katika mochari ya City, Nairobi baada ya kutafutwa kwa zaidi ya wiki moja na familia yake.

Kilichoibuka baada ya upasuaji wa mwili huo ni kwamba aliuawa kinyama -kabla ya kutupwa barabarani na kukanyangwa na magari.

Hilo si tukio la kwanza, ila ni mtindo unaoonekana kuendelea nchini. Mwezi uliopita, mwanafunzi Cariltln Maina alipatikana ameuawa kitatili katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi, ambapo mwili wake ulikuwa na majeraha ya risasi.

Ripoti zilisema kwamba mwanafunzi huyo, ambaye alikuwa akisomea katika Chuo Kikuu cha Leeds, Uingereza, aliuawa na polisi kwa kutuhumiwa kuwa miongoni mwa kundi la vijana waliokuwa wakiwahangaisha wakazi.

Hayo ni matukio mawili tu katika msururu wa visa ambavyo vimekuwa vikitokea nchini tangu mwaka 1963.

Waliouawa ni wengi, ila hakuna juhudi za kuwatambua waliohusika zilizofaulu.

Miongoni mwa wale ambao wameuawa kikatili ni mwanasiasa Josiah Mwangi Kariuki, maarufu kama ‘JM’ aliyeuawa Machi 1975 na mwili wake kutupwa katika Msitu wa Ngong. Bw Kariuki alikuwa mbunge wa Nyandarua Kaskazini na mkosoaji mkubwa wa utawala wa uongozi wa Mzee Jomo Kenyatta.

Wengine ni mwanasiasa Tom Mboya (1969), mwanaharakati Pio Gama Pinto (1963), aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni Robert Ouko (1990) kati ya wengine wengi. Katika mauaji ya JM, kamati maalum ya Bunge ambayo iliongozwa na mwanasiasa Elijah Mwangale ilishindwa kubaini wale waliohusika katika mauaji hayo.

Hali iyo hiyo ndiyo imeandama chunguzi nyingine nyingi ambazo zimeendeshwa kujaribu kutegua kitendawili cha wahusika wakuu.

Kwa hayo basi, ni wakati mwafaka kwa serikali kujaribu kuhakikisha kuwa mtindo huu umeisha, kwa kuwahusisha wachunguzi wa kimataifa, ikiwa wale walio humu nchini watashindwa kubaini wanaohusika katika mauaji hayo.

Kilicho dhahiri ni kwamba katika baadhi ya matukio hayo, polisi wamekuwa wakihusishwa. Polisi pia wametajwa kuhongwa na wanasiasa ili kuwaua baadhi ya mahasimu ama wakosoaji wao.

Cha kushangaza ni kwamba, licha ya mageuzi makubwa katika idara ya polisi kama vile kuanzishwa kwa Mamlaka Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi (IPOA) ukatili wao dhidi ya umma haujapungua.

Hilo lilidhihirika wazi kwenye ghasia za baada ya uchaguzi tata wa 2007 na 2017.

Mnamo 2007, kutowajibika kwa polisi ndiko kunakotajwa kuchangia aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Polisi Hussein Mohamed kufunguliwa mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na watu wengine watano.

Kutowajibika kwao pia kulitajwa kuchangia vifo vya watu kadhaa baada ya uchaguzi wa 2017. Ili kuepuka mauaji kama haya, umefikia wakati ambapo mauaji hayo yanafaa kuchunguzwa na kukabiliwa kisheria.

[email protected]