Makala

WANDERI: Valentino ni hadaa ya usasa inayodunisha tamaduni zetu

February 15th, 2018 2 min read

Wakazi wa jiji la Nairobi wakinunua maua kwa wapendwa wao Valentino Dei Februari 14, 2018. Picha/ Bernardine Mutanu

Na WANDERI KAMAU

Kwa ufupi:

  • Valentino ni hadaa ya usasa. Ni mambo ya kigeni ambayo ni mwigo wa kigeni
  • Mapenzi ya sasa ni kama kamari. ‘Mshindi’ mmoja husherehekea huku mamilioni ya walalahoi wakiomboleza
  • Ni siku hii ambapo mabikra hupoteza ubikra wao huku mateka wa ngono wakipata uzoefu
  • Mwigo huu wa tamaduni za uzunguni umetuzalia uozo wa kimaadili tunaoshuhudia kwa sasa

SIKU ya Valentino ambayo iliadhimishwa Jumatano hujaa vituko na vizushi vya kasumba iitwayo ‘mapenzi.’

Ni kasumba ambayo kwa namna moja, imedunisha tamaduni zetu na kutufanya kama vinyago tu!

Mwanadamu hugeuka kama kwamba kavuta bangi ama kanywa pombe ndipo akalewa na uzushi huo.

Kwa mantiki ya Kiafrika, Valentino ni hadaa ya usasa. Ni mambo ya kigeni aliyojiwekelea Mwafrika, ambayo ni mwigo wa kigeni na ukinzano mkuu wa maisha ya Kiafrika.

Kuna maswali kadhaa: Mbona iwe Februari 14 ndipo ‘mapenzi’ hudhihirika? Inamaanisha kwamba siku zingine hayapo? Tofauti ya siku hii na zinginezo ni ipi? Mbona uzushi huu unakumbatiwa na kizazi cha sasa?

Naam, haya ni baadhi ya maswali ambayo yangali yanatafutiwa majibu, wakati kila mmoja anajifumba upofu ‘kusherehekea’ Valentino. Kwangu, mapenzi ya usasa ni utapeli mtupu.

 

Kamari ya mapenzi

Ni mfano wa biashara ya kishetani ambayo imefichwa na hadaa kuu. Mapenzi ya sasa ni kama mchezo wa kamari, ambapo ‘mshindi’ mmoja husherehekea, wakati mamilioni ya walalahoi wakiomboleza kwa kulaghaiwa jasho lao.

Ni dhahiri kwa kila mmoja kwamba mapenzi yalipoteza thamani yake zamani sana. Ujio wa usasa ulifanana na gharika kali, ambalo lilisomba thamani yake, ambayo ilizingatiwa na mababu zetu.

Siku hii ni mfano wa Siku ya Kiyama. Ni Siku ya Kicheko kwa Shetani au Mahoka Mkuu. Ni siku iliyolaaniwa. Ni siku ambapo dhambi huitawala dunia.

Ni siku ambayo Shetani na malaika wake husherehekea Jehanamu kwa kupata wingi wa wafuasi.

Wanaume walio katika ndoa hupata ajali. Wengine hutumwa safari za mbali kazini mwao. Ni siku hii ambapo mabikra hupoteza ubikra wao. Ni siku ambapo mabumbumbu wa ngono hupata uzoefu.

 

Maombolezo

Siku ii hii ndipo malimbukeni wa mihadarati huwa wazoefu. Ni siku ambapo wamilikio vyumba vya malazi ya kukodisha husherehekea.
Hivyo, ni siku ya Maombolezo Makuu. Hadaa itaitawala dunia.

Mwigo huu wa tamaduni za Kimagharibi ndiyo umetuzalia mmomonyoko wa kimaadili tunaoshuhudia kwa sasa, hasa miongoni mwa wanandoa.

Hivyo, wakati kila mtu anang’ang’ana kununua, maua, nimeamua kuandika nyaraka hii ya maombolezo, kulilia upofu aliyojivika mwanadamu.

Sitasherehekea. Sitoitambua. Nitakuwa kimya, katika dua nikimwomwa Muumba kuirejeshea jamii yetu utambuzi wa thamani ya kuzingatia upendo kila siku!

 

Baruapepe: [email protected]