MakalaSiasa

WANDERI: Vijana ndio watakaosaidia kuleta mwamko mpya Afrika

April 4th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

MNAMO Ijumaa iliyopita, baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta walizua rabsha baada ya kufahamu kwamba Rais Yoweri Museveni wa Uganda angetoa hotuba maalum chuoni humo.

Wanafunzi hao walishikilia hawangempa kiongozi huyo nafasi ya kuhutubu, ikizingatiwa kwamba amekuwa akitumia mamlaka yake kuwahujumu vijana, hasa mwanamuziki Bobi Wine.

Na ingawa hatimaye alifaulu kutoa hotuba yake, kilicho dhahiri ni kuwa vijana wanaendelea kupata mzinduko kuhusu ukatili na dhuluma zinazoendelezwa na tawala nyingi za sasa barani Afrika.

Nchini Uganda, mwamko wa sasa wa vijana unaongozwa na mwanamuziki huyo, ambaye pia ni mbunge wa eneo la Kyadondo Mashariki, Bobi Wine.

Mbunge huyo ameongoza kampeni nyingi ambapo wabunge kadhaa wa Upinzani wameibuka washindi kutokana na juhudi zake.

Wine ametangaza atawania urais kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika 2021. Ameeleza kuwa msukumo wake mkuu ni kuikomboa Uganda kutoka kwa utumwa wa utawala wa Rais Museveni, kwani amekataa kuondoka uongozini tangu 1986 alipochukua uongozi.

Nchini Kenya, uchaguzi mkuu umepangiwa kufanyika Desemba 2022. Hili linamaanisha kuwa chaguzi hizi mbili zitakuwa na umuhimu mkubwa wa kisiasa katika nchi hizo mbili.

Kenya kwa sasa inamezwa mzima mzima na msururu wa sakata za rushwa. Mabilioni ya fedha yanapotelea mikononi mwa watu wachache, na uongozi wa Rais Uhuru Kenyatta unaonekana kutofanya lolote kuhusu sakata hizo.

Usawiri wa kina unaonyesha chaguzi hizi mbili zina umuhimu mkubwa wa kisiasa kwa ukombozi wa kimfumo wa mataifa haya mawili.

Hii itakuwa nafasi ya Uganda kujikomboa kutoka kwa udhalimu wa Museveni, huku Kenya ikipata nafasi mwafaka wa kujikomboa kutoka kwa minyororo ya ukiritimba wa kisiasa wa familia za Mzee Jomo Kenyatta na Jaramogi Oginga Odinga.

Mwanawe Mzee Kenyatta, ndiye rais wa nne wa Kenya, huku mwanawe Jaramogi, Raila Odinga, akiwa kiongozi wa Upinzani.

Kimsingi, huu ni utumwa wa kisiasa ambao kwa namna moja umelizalia Kenya matatizo mengi yanayoikumba kwa sasa.

Rais Kenyatta ameshindwa kabisa kuzima saratani ya ufisadi, huku Bw Odinga akilaumiwa kutowasaidia wafuasi wake, licha ya kuhudumu serikalini kwa zaidi ya miongo miwili.

Kwa sasa, wawili hao wanawafumba Wakenya macho kupitia “mwafaka wa kisiasa”—wanaoutaja kuwa “mapambazuko mapya ya kisiasa” kwa mustakabali wa Kenya.

Je, mbona mwafaka huo umekosa kubuni nafasi za ajira kwa maelfu ya vijana wanaohitimu kutoka asasi mbalimbali za umma?

Mbona mwafaka huo umekosa kubuni mazingira yafaayo ya kibiashara? Mbona wananchi wanaendelea kufariki kutokana na njaa?

Haya ni maswali magumu ambayo vijana wanapaswa kujiuliza, hasa siasa za urithi wa Rais Kenyatta zinapoendelea kushika kasi.

Imefikia wakati vijana wote barani Afrika kuungana kuzipindua tawala kandamizi ambazo lengo lao kuu limekuwa ni kuwalinda na kuzitajirisha familia chache.