Habari Mseto

Wanafunzi wadaiwa kumuua mwalimu kwenye purukushani za baa

August 30th, 2018 2 min read

NA ELIZABETH OJINA 

WANAFUNZI watatu wamekamatwa Alhamisi kwa madai ya kumkatakata mwalimu wa shule ya upili hadi kufa eneo la Nyakach, kaunti ya Kisumu.

Washukiwa ni wanafunzi wawili wa kidato cha nne shule za upili za Wang’a Pala na Ramba wakishikiriana na mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi.

YALIYOTOKEA

Mwathiriwa, Manasseh Omarami, aliye na umri wa miaka 41 ambaye ni mwalimu katika Shule ya Sekondari ya Guu alishambuliwa usiku wa Jumatano karibu na baa ya Heraremo  karibu na soko la Nyamaroke mjini Koguta.

Akiwa na marafiki zake Steve Ondong’a na Johnson Alai, Bw Omarami alikuwa amevurugana na wanafunzi hao.

Bw Alai ambaye amelazwa kwenye hospitali ya misheni ya Nyabondo alisema walikuwa wakijivinjari kwa vileo kwenye baa hiyo wakati wanafunzi hao waliingia na kuanza vituko. Alisema walikuwa wametoka Sondu.

Katika kisa kama hicho wanakijiji huua mshukiwa na kumteketeza. Mshukiwa alisaidia polisi baada ya mauaji ya mwanamke Meru.

“Tulipokuwa tukiongea nao, walitwambia hawaguziki. Baadaye, mfanyikazi wa baa aliwafukuza. Walirudi lakini mfanyikazi huyo alidinda kuwauzia.Ndipo wakaondoka kwa fujo,” akasema Bw Alai.

Wakiwa na marafiki zake, Omarani aliondoka mwendo wa saa nne usiku na kushambuliwa mita kadhaa mbali na soko baada ya pikipiki yao kuharibika.

“Katika harakati za kutengeneza pikipiki, tulishambuliwa kwa mapanga. Ndipo nikapoteza fahamu kwa muda. Nilipoamka, niligundua nilikuwa nimekatwa vibaya kichwani.”

Bwana Ondong’a alipelekwa katika hospitali ya Jaramogi Oginga Odinga, ambapo daktari mkuu Peter Okoth alisema hayuko hatarini.

“Mgonjwa aliletwa usiku. Alishughulikiwa katika idara ya majeruhi maanake alikuwa amekatwa vibaya kichwani na uso lakini hayuko hatarini kwa sasa,” alinukuu Daktari Okoth.

Kamanda wa polisi kaunti ya Kisumu Job Boronjo alisema kuwa mwalimu alifia pale unyama huo ulipokuwa ukitekelezwa.

“Uchunguzi bado unaendelea…na wahusika watakamatwa hivi karibuni.”

USALAMA ZAIDI

Walimu pamoja na katibu mkuu wa Kuppet kaunti ya Kisumu Bw Zablon Awange, walikashifu mauaji hayo wakisema usalama wafaa kutekelezwa kwa hali ya juu eneo la Nyakach.

“Tunataka waliohusika kutekeleza unyama huo washikwe upesi iwezekanavyo.

Uchunguzi ufaao utekelezwe kuhakikisha haki imetendeka. Kila kifaacho kufanywa lazima kifanyike ili hao wahalifu wapate kuhukumiwa,” alihimiza Bw Awange.

Mwili wa Marehemu Bw Omarami ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Misheni Nyabondo.