Michezo

Wanga ataka FKF ihimize na ihamasishe wanasoka kuhusu umuhimu wa kuwekeza kabla ya kustaafu

July 15th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA wa Kakamega Homeboyz, Allan Wanga, ametaka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kutoa mafunzo maalumu ya kushauri wachezaji kuhusu jinsi ya kuendesha biashara na kuwekeza katika masuala mengine kwa minajili ya kujiandaa kwa maisha baada ya kustaafu soka.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Harambee Stars ameonya kwamba japo kabumbu ni taaluma iliyo na tija kwa mwanasoka yeyote aliyemakinika, mafao yake ni ya kipindi kifupi. Hivyo, itakuwa vyema iwapo FKF itatoa majukwaa ya kushauri masogora kuhusu jinsi ya kumudu maisha na kukimu mahitaji mengine ya kimsingi baada ya kuangika daluga zao ulingoni.

Kwa mtazamo wa Wanga, kumekuwa na visa vingi vya wanasoka wa Kenya waliowahi kutamba katika enzi zao kuishi maisha ya kusikitisha baada ya kustaafu.

“Haya ni matukio ambayo yanaweza kupunguzwa au kuzuiliwa kabisa kupitia ushauri unaofaa. Husikitisha sana kuwaona baadhi ya wachezaji waliokuwa wa haiba kubwa nyakati zao, ambao wanastahili kuwa vielelezo bora kwa chipukizi wanaoinukia kitaaluma, wakiishia kuwa omba-omba,” akatanguliza Wanga.

“Mbali na kucheza mpira, mafunzo ya sampuli hiyo yatawahamasisha kuanza kuwekeza katika masuala mengine, hasa biashara ambazo watasalia kuzitegemea baada ya kuondoka kwenye ulingo wa soka. Iwapo kuna wachezaji waliokamilisha elimu ya sekondari na wakafaulu vyema katika mitihani, basi mafunzo hayo yatawapa changamoto ya kujiendeleza hata zaidi kimasomo ili wapate maarifa na ujuzi utakaowafaa baada ya miaka ya kucheza soka kutimia,” akaongeza.

Mbali na kuchezea Homeboyz, Wanga kwa sasa ni Afisa wa Michezo katika Kaunti ya Kakamega.

Wito wake kwa FKF inatolewa siku chache baada ya bingwa wa dunia katika mbio za mita 5,000 Hellen Obiri kuwasihi wanariadha wenzake kuanza pia kuwekeza kwingi ili wawe watu wa kujitegemea baada ya kustaafu.

Tangu Machi 2020, shughuli zote za michezo zilisitishwa humu nchini kutokana na janga la corona. Hilo limekuwa pigo kubwa kwa wanamichezo wengi waliokuwa wakitegemea majukwaa ya sampuli hiyo pekee kama kitega-uchumi.

Wanga amewahi pia kuvalia jezi za klabu za Tusker, AFC Leopards, Azam FC (Tanzania), Al-Merreikh SC (Sudan), Hoang Anh Gia Lai (Vietman), FK Baku (Azerbaijan) na Petro Atletico (Angola).