Michezo

Wanga, Kasumba sako kwa bako vita vya kuibuka mfungaji bora Ligi Kuu ya Kenya

May 7th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

ZIKISALIA mechi sita Ligi Kuu ya msimu 2018-2019 itamatike, mvamizi Allan Wanga anasalia katika nafasi nzuri ya kutwaa taji la mfungaji bora baada ya kufikisha magoli 16 alipopachika penati klabu yake ya Kakamega Homeboyz ikizamisha Kariobangi Sharks 3-0 Mei 5, 2019.

Katika orodha ya wafungaji 114 kwenye ligi hii ya klabu 18 kwa alama 1.13, pointi 0.07 mbele ya Mganda Umaru Kasumba anayechezea Sofapaka.

Wamekuwa sako kwa bako katika nafasi ya kwanza tangu mechi za raundi ya 27 baada ya Kasumba kuondoa mwanajeshi Enosh Ochieng’ kutoka nafasi ya pili.

Kasumba alihakikisha anasalia katika vita vya kuwania tuzo ya mfungaji bora ya Sh500, 000 baada ya kufumia waajiri wake bao katika mechi iliyopita dhidi ya Tusker ambayo Sofapaka ilitupa uongozi wa mabao 2-0 na kukabwa 2-2.

Ochieng’ kutoka Ulinzi Stars ameona lango mara 15, ingawa hakubahatika kuimarisha magoli yake wanajeshi hao walipopepeta Nzoia Sugar 1-0 Jumatatu.

Cliff Nyakeya alisalia katika nafasi ya nne akifikisha mabao 11 alipofungia Mathare United bao moja ikikanyaga AFC Leopards 2-0 uwanjani Bukhungu mnamo Mei 5.

Derrick Otanga kutoka SoNy Sugar ni mchezaji mwingine aliyefaulu kufikisha mabao 10 na kuendelea baada ya kufungia wanasukari hao mabao 10.

SoNy haikuona lango katika mechi za raundi ya 28 pale ilipoumiza nyasi bure katika sare tasa dhidi ya wenyeji wake Zoo mjini Kericho. Mfungaji anayeongoza kufungia mabingwa watetezi Gor Mahia, ambao pia wamo mbioni kushinda ligi kwa mara ya 18, ni Nicholas Kipkirui. Ametikisa nyavu mara saba.

Whyvonne Isuza pia amefungia Leopards idadi sawa ya mabao. Kariobangi Sharks, ambayo ilitoa mfungaji bora katika misimu miwili iliyopita kupitia kwa Masoud Juma mwaka 2017 (mabao 17) na Eric Kapaito mwaka 2018 (16), msimu huu inaelekea kupoteza taji hili. Mchezaji anayeongoza kufungia Sharks mabao ni Sydney Lokale.

Amecheka na nyavu mara sita. Mfungaji bora katika historia ya timu ya taifa ya Kenya, Dennis Oliech amejaza wavuni mabao matano. Hata hivyo, msimu wa Oliech, ambaye alifungia Harambee Stars mabao 34 katika mechi 72 kati ya mwaka 2002 na 2016, ulikatizwa ghafla baada ya kuumia vibaya mkono dhidi ya Western Stima mnamo Mei 5. Inasemekana atakuwa mkekani miezi sita.

Kapaito, ambaye aliibuka mchezaji bora wa mwaka 2018, ametikisa nyavu mara nne pekee msimu huu.

Wachezaji bora wa mwaka 2016 Kenneth Muguna na mwaka 2017 Michael Madoya wamefungia Gor Mahia na Tusker mabao mawili na goli moja mtawalia.

Wanga,33, atakuwa mchezaji wa kwanza wa Homeboyz kuibuka mfungaji akimaliza juu ya jedwali la wafungaji. Homeboyz kutoka kaunti ya Kakamega ilianzishwa mwaka 2010 na kuingia Ligi Kuu mwaka 2013.

Ilitemwa mwisho wa msimu 2013 kabla ya kujikakamua na kurejea katika ngazi ya juu ya ligi mwaka 2015.